Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amewataka Mshauri Mwelekezi kampuni ya Inter Consultant Ltd na mjenzi kampuni ya MCB Co. Ltd kutoka Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) kukamilisha kwa wakati ujenzi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Geita kama ilivyopangwa.

Prof. Msanjila ameyasema hayo leo tarehe 25 Oktoba, 2021 wakati wakusaini Mkataba wa ujenzi na Mkataba wa Mshauri Mwelekezi wa ujenzi wa ofisi hiyo  katika tukio lililofanyika katika ofisi za Wizara zilizopo mji wa Magufuli- Mtumba Jijini Dodoma.

Awali, Prof. Msanjila alitoa pongezi kwa kampuni hizo kuaminiwa na kushinda zabuni ya ujenzi wa ofisi hiyo baada ya mchakato wake kukamilika na kuwataka kwenda kwa kasi ili kukamilisha mradi huo kwa wakati.

Pamoja na hayo, Prof. Msanjila amewataka wataalamu hao kutosita kufanya mawasiliano na ofisi yake pindi watakapokutana na changamoto yoyote wakati wa utekelezaji wa mradi huo ili kusaidia katika kutatua changamoto hizo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya MCB, Ivor Ndimbo amemhakikishia Katibu Mkuu, Prof. Msanjila na ujumbe uliohudhuria utiaji saini wa mikataba hiyo kutekeleza mradi huo kwa uadilifu mkubwa na kufuata taratibu zote za manunuzi ya umma kama Sheria ya Manunuzi inavyoelekeza.

“Hatutakuangusha, hii ni mara ya pili kufanya kazi na Mshauri Mwelekezi binafsi (independent Consultant) tunaahidi kufanya kazi hii kwa weledi mkubwa,” amesisitiza Mhandisi Ndimbo.

Pia, Mhandisi Ndimbo amemhakikishia Mshauri Mwelekezi kumpa ushirikiano wa kutosha na kumtaka kutosita kuchukua hatua madhubuti pindi atakapobaini kuwepo kwa ukiukwaji wa taratibu wakati wote wa utekelezaji wa mradi huo.

Vilevile mshauri Mwelekezi Arch. Beno Matata amekiri kuwa, muda wa utekelezaji wa mradi si rafiki, hivyo amewashauri wahusika wa ujenzi wa mradi huo kunuia kutekeleza mradi huo kwa wakati na kusisitiza uwepo wa ushirikiano mkubwa ili kufikia malengo ya Wizara na kampuni hizo kwa ujumla.

Akielezea wito wa Kuwasilisha changamoto wanazokutana nazo wakati wa utekelezaji wa mradi huo kama ulivyotolewa na Prof. Msanjila, Arch. Matata ameahidi kuwasiliana na wizara pindi wanapokutana na changamoto yeyote wakati wa utekelezaji wa mradi husika.

Wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba na Viongozi wengine wa Wizara na Tume ya Madini.

Ujenzi wa Ofisi ya Madini Geita unatarajia kukamilika katika Mwaka wa Fedha 2021/22.

 

Share To:

Post A Comment: