Wednesday, 20 October 2021

NAIBU WAZIRI ELIMU AKAGUA ENEO LA CHUO KISARAWE

 


Na WyEST


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (Mb) ametembelea kukagua eneo kitakapojengwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kisarawe lililopo Kata ya Mzenga Wilayani Kisarawe Mkoani Pwani ambacho ujenzi wake unatarajiwa kuanza Novemba 2021.


Akiwa hapo ameelezea kufurahishwa na jitihada zilizofanywa na Uongozi wa Wilaya ya Kisarawe za kuwashirikisha wananchi wa Kata ya Mzenga katika kusafisha eneo la ujenzi kwa gharama ya Shilingi milioni 3 kutoka milioni 26 iliyotajwa awali.


Aidha, Mhe. Kipanga amewataka wasimamizi wa ujenzi kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Kisarawe kuhakikisha mradi unatekelezeka kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati.


"Mradi huu ni wetu sote na chuo hiki kitatoa elimu kwa watoto wetu wa eneo hili, hivyo niwaombe wote mshirikiane kuhakikisha mradi unatekelezwa vizuri ili matokeo yanayotarajiwa yaweze kufikiwa," amesema Mhe. Kipanga.


Akitoa taarifa ya Mradi huo, Mshauri Elekezi kutoka Chuo cha Ufundi Arusha, Nestory Robert amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa chuo hicho utahusisha majengo 11 yatakayogharimu Shilingi bilioni 1.04 na utakamilika ndani ya miezi sita.


Ameyataja majengo hayo kuwa ni jengo la Utawala, madarasa, karakana 3, bwalo la chakula, vyoo, mabweni 2 yenye uwezo wa kuchukua wanachuo 160, nyumba ya mkuu wa chuo pamoja na nyumba 2 za watumishi.


Naye Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kisarawe, Joseph Mugeta amesema chuo hicho kwa sasa kinatumia majengo ya Kanisa la KKKT yaliyopo Kisarawe mjini.


Amesema chuo chake kwa sasa kina jumla ya wanachuo 518 kati yao 232 ni wa kozi fupi. Amezitaja kozi zinazotolewa chuoni hapo kuwa ni ufundi magari, ushonaji, upishi, uchomeleaji vyuma na uwashi.


No comments:

Post a Comment