Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jaji Joseph Sinde Warioba amekemea vikali masuala ya Ukabila, Ukanda na Uvyama maneno ambayo yameanza kusikika  nchini, huku akisisitiza Watanzania kuwa kitu kimoja.


Jaji Warioba ametoa Kauli hiyo hii leo wakati akizungumza kwenye kongamano la Kumbukizi ya miaka 22 ya Kifo Cha Baba wa Taifa Mwalimu, J.K. Nyerere, katika Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kampasi ya  kivukoni jijini Dar es Salaam.


“Udini unaanza kuzungumzwa, ukabila unazungumzwa, Uvyama unaanza kuzungumzwa

Ile misingi ambayo ilijengwa na Baba wa Taifa inaanza kuvunjwa, ni wajibu wetu Watanzania kukemea wale wote wanaotaka kuleta ukabila, udini na ukanda  hivyo ni lazima Watanzania tuwe kitu kimoja na tujivunie Utanzania wetu”,alisisitiza Jaji mstaafu Mzee Warioba.


Jaji Warioba amesema enzi za uhai wa Mwalimu Nyerere hakupenda kutukuzwa kwa majina ya Uheshimiwa, Ukuu, Mtukufu,kwa vile aliamnini binadamu wote ni Sawa.


Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mwenywkiti wa Bodi ya Chuo Mhe. Stephen Wasira amemuelezea Baba wa Taifa kuwa alikuwa ni Kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya kutetea maslahi ya Watanzania, alikemea Udini, ukabila na aliamini kuwa binadamu wote ni ndugu.


“ Baba wa Taifa aliamini katika Umoja, Usawa na Utu na ndiyo maana hata ukiangalia mada kuu ambayo inajadiliwa katika kongamano hilo inasema, MAONO YA MWALIMU NYERERE KATIKA UONGOZI, MAADILI, UMOJA, NA AMANI KWA MAENDELEO YA JAMII”


Mkuu wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila amesema Chuo kinatoa mafunzo ya uongozi, maadili, uzalendo, Chuo pia kinafanya tafiti ambazo zinatatua changamoto katika jamii ,  kinatoa ushauri kwa Sekta binafsi,  kinatoa na pia  kozi ambazo zinakidhi mahitaji ya kila ngazi kuanzia kijiji,Wilaya, Mkoa na Taifa.


Prof. Mwakalila amesema Chuo kila mwaka kimekuwa kinaadhimisha makongamano matatu ambayo Lengo la makongamano hayo ni sehemu ya kuwaenzi waasisi wa Taifa ambao ni Hayati Mwalimu J. K. Nyerere na Sheikh Abeid Karume.


Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Bara Mhe. Philip Mangula amewataka viongozi wanaopewa dhamana kuhakikisha wanafanya kazi ya kuwatumikia wananchi kwa kuzingatia umoja na mshikamano kama alivyokuwa akiishi Baba wa Taifa.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Mzee Joseph Butiku amesema Baba  wa Taifa  aliamini kuwa watu wote ni Sawa na haki zote ni Sawa, hivyo lazima Kila mmoja aheshimu utu wa kila mtu.


Imetolewa na:

KITENGO CHA HABARI NA UHUSIANO

CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE 

12.10.2021

Share To:

Post A Comment: