Mwenyekiti
wa mtaa wa Komoto Paskali Petro amesema atajiuzulu endapo mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji wa Babati hatozipeleka fedha za fidia shilingi
milioni 132 zilizolipwa na TANESCO kupisha Mradi wa gesi uliopita katika
eneo la shule ya Msingi na Sekondari Komoto zilizopo katika mtaa huo.
Mwenyekiti
huyo ameeleza hayo mbele ya mkuu wa mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere
aliyeambatana na mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange kusikiliza
malalamiko ya viongozi na wananchi wa Mtaa wa Komoto kuhusu fedha hizo.
Amehoji
kwanini mkurugenzi akae na madiwani kugawa fedha za mtaa wa Komoto,
kwamba jambo hilo halikubaliki kwani shule ni mali ya Umma ambao ni
wananchi wa mtaa huo?
“Kama
kuna vinginevyo basi leo niambiwe kwa maandishi ili niwaambie wananchi
wa Mtaa wa Komoto kuwa shule ni mali za Mkurugenzi, na kauli hii
mkurugenzi aliwahi kunitamkia kwamba shule ni mali yangu na ninaweza
kupeleka pesa popote ninapotaka”alisisitiza Mwenyekiti huyo
Ameongeza
kuwa shule hiyo ya Msingi Zaidi ya miaka kumi haijawahi kupatiwa ruzuku
aidha kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri au serikali kuu.
”Iweje leo mkurugenzi atumie fedha ambazo zimepita kwenye eneo la
shule,imeathiri eneo la shule,hiki kitu hakiwezekani”
Amesema
kama atapatiwa taarifa kwa maandishi yupo radhi na hatosumbuka na
kwamba atawaambia wananchi kuanzia leo naomba nijiuzulu niachane na hizi
shughuli ili serikali ifanye inayoyajua kwa kuwa wamefanyiwa uonevu.
“Haiwezekani
watoto wetu wanakaa kwenye vumbi,mbao zinawaangukia hata hela ya
ukarabati tusipate, naomba kupewa kwa maandishi na nilishwahi kumwambia
DAS anipe maandishi kwamba shule kwamba shule ni mali ya
mkurugenzi,ameshindwa kunipa” alimwambia Mkuu wa mkoa
Akitoa
taarifa kwa mkuu wa mkoa na wajumbe wa Mtaa wa Komoto kwa niaba ya
Mkurugenzi wa Mji wa Babati Faustine Masunga amesema fedha hizo
ziliingia kwenye akaunti ya Halmashauri ya Mji wa Babati na
zimeshatumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Masunga
amesema mkurugenzi aliziwasilisha taarifa ya fedha hizo kwenye vikao
vya Halmashauri na baadae baraza la Madiwani kuamua ambapo fedha hizo za
fidia ziligawanywa kwenye kata mbalimbali ambapo kata ya Babati ilipewa
Milioni 30,Bagara Milioni 30,Bagara Milioni 30,Maisaka Milioni
50,Mutuka Milioni 30, Sigino Milioni 30,Bonga Milioni 30,Singe Milioni
30 na Nangara Milioni 50.
Baadhi
ya wajumbe katika serikali ya mtaa huo wamesema fedha za fidia
zimepelekwa sehemu ambazo sio sahihi na kwamba zingepaswa zielekezwe
moja kwa moja katika mtaa huo ili zisaidie kukarabati shule hizo mbili
zenye upungufu wa madarasa na miundombinu mingine.
Mkuu
wa mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere amewataka Viongozi wa mitaa na
vijiji katika mkoa huo ambao wamepitiwa na miradi kwenye maeneo yao
yenye taasisi, wafuatilie fidia zao wanazostahili kulipwa kwa kufika
katika ofisi za mkuu wa wilaya husika ili kufanyiwa kazi.
“Msiache
kuja kufuatilia fedha za fidia,wito wangu ni kwamba viongozi wa
mitaa,vijiji mkoa wote wa Manyara kama kuna fidia inatakiwa kutolewa na
hamjapewa, msikate tamaa,fikeni toeni taarifa ofisi ya DC wa wilaya
husika,matumaini yangu litafanyiwa kazi na endapo itachukua muda mrefu
njooni kwangu” alisema Nyerere
Makongoro
Nyerere akizungumzia mzozo uliopo Komoto baada ya fedha za fidia
walizopaswa kupatiwa kugawanywa katika maeneo mengine,amesema taarifa
alizipata kupitia viongozi wa mtaa huo na anaendelea kuzifanyia kazi
Licha
ya fedha hizo kutolewa kwa ajili ya shule mbili za Komoto Sekondari na
Komoto Msingi wajumbe hao wameshangazwa na kitendo cha kugawanywa na
kupewa shilingi milioni 30 kinyume na matarajio yao.
Fidia
iliyolipwa na TANESCO ni milioni 132 ambapo Shule ya Sekondari Komoto
ilipaswa kulipwa shilingi Milioni 103 huku ya msingi ikitakiwa kupewa
Milioni 29.
Post A Comment: