Tuesday, 5 October 2021

FAHAMU : Maajabu 10 ya Hifadhi ya Arusha Nationa Park

 Hifadhi ya Taifa ya Arusha inahusisha Mlima Meru, mlima maarufu wa volcano wenye urefu wa meta 4566 (futi 14,977 au kilometa 4.6) kutoka usawa wa bahari, na ipo katika Mkoa wa Arusha, kaskazini mashariki mwa Tanzania.


Hifadhi hii ni ndogo iliyoanzishwa rasmi mwaka 1960, ikiwa na eneo la kilometa za mraba 137 tu, inavutia ikiwa na aina tofauti ya uoto katika maeneo matatu. Magharibi, Kasoko ya Meru (Meru Crater) kuna Mto Jekukumia; kilele cha Mlima Meru kinapatikana hapa. Kasoko ya Ngurdoto (Ngurdoto Crater) upande wa kusini-mashariki ni eneo la nyasi nyingi. Maziwa madogo yenye vina vifupi ya Momella yaliyojaa magadi kaskazini mashariki mwa hifadhi hii yanatofautiana kwa rangi na ni maarufu kwa aina nyingi za ndege wanaopatikana huko.

Lango kuu la kuingilia Hifadhi ya Taifa ya Arusha.

Mlima Meru ndio mlima wa pili kwa urefu Tanzania baada ya Mlima Kilimanjaro, ambao uko takriban kilometa 70 tu mashariki na unaonekana vizuri ukiwa kwenye hifadhi hii ya Arusha. Hifadhi ya Taifa ya Arusha inapatikana katika muhimili wa kilometa 300 wa hifadhi za taifa maarufu barani Afrika, kuanzia Serengeti na Kasoko ya Ngorongoro (Ngorongoro Crater) upande wa maharibi na Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro upande wa mashariki.

Usitishwe na viwango hivi, ni gharama nafuu sana kwa Mtanzania kutembelea hifadhi zetu. Utamu wa ngoma ingia ucheze ati.

Hifadhi hii ipo kilometa chache tu kaskazini mashariki mwa Jiji la Arusha, ingawa lango kuu la kuingilia lipo umbali wa kilometa 25 mashariki mwa jiji. Pia iko umbali wa kilometa 58 tu kutoka Moshi mjini na kilometa 35 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

WAMERU WAKATIZA KWA MIGUU

Ukiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha siyo tu utafurahia kuangalia mandhari nzuri ya asili iliyosheheni hayawani na ndege wa kila namna, bali utajifunza na historia ya wakazi wa maeneo hayo, hasa Wameru na Waarusha. Wameru ambao wanakaa katika miteremko ya Mlima Meru walihamia hapo zaidi ya miaka 300 iliyopita na kwa sasa wanadhaniwa kuwa idadi yao ni milioni 2.

Wameru hawa wanahusiana jina tu na wale wa Kenya, lakini historia yao ni tofauti. Hawa wa Tanzania wanasemekana kuwasili kwenye miteremko ya mlima huo mkubwa wakitokea kwenye Milima ya Usambara katika Mkoa wa Tanga miaka 300 iliyopita, waliwasili pamoja na Wachaga-Wamachame wa kwanza. Walipowasili katika miteremko ya mlima kusini-mashariki waliwakuta jamii ya wawindaji waliofahamika kama Wakoningo, ambao walizamia kwenye jamii ya Wameru. Waarusha wao asili yao ni Wapare na walifikia Arusha Chini, lakini wakaathiriwa na tamaduni za Kimasai na kushawishiwa kuishi upande wa magharibi uliko mji wa Arusha.

Wamasai nao walikuwa kwenye mteremko wa mlima wakifuga kama ilivyokuwa kwa Waarusha. Katika miaka ya 1830 Wameru walipoteza ng’ombe wao wengi kutokana na vita dhidi ya Wamasai waliotaka kuhodhi mifugo yote pamoja na maeneo ya malisho. Wameru wakakimbilia upande wa pili wa mlima kutafuta hifadhi.

Kwa kutambua kwamba mlima na misitu ndiyo iliyowaokoa, Wameru tangu enzi hizo wamekuwa wahifadhi wazuri na hawakuweza kuharibu mazingira huku wakiendelea na kilimo cha mazao mbalimbali, ikiwemo kahawa. Ni watunzaji wazuri wa ardhi kutokana na historia ya eneo hilo ambalo limekuwa na migogoro ya ardhi tangu enzi za utawala wa Mjerumani.

Hata kabla haijatangaza eneo hilo kuwa hifadhi mwaka 1960, Wameru wamekuwa wakikatiza kwa miguu msituni kutoka Arumeru kwenda upande wa kaskazini hadi Ngarenanyuki na vijiji vingine vya huko. Barabara kuu inayokatiza kutoka kwenye Lango la Ngongongare (kwa Kimasai ni Engong Engare – Eneo la Majimaji) upande wa kusini kuelekea kaskazini kupitia geti la Momella, inaelezwa kwamba inakwenda mpaka Kenya.


Kwa hali hiyo, siyo ajabu ukifika kwenye mageti hayo au hata ukiwa hifadhini ukakutana na bodaboda au watu wanaotembea kwa miguu, kwani ndiyo njia kuu wanayoitumia wananchi wa huko, hasa wa upande wa kaskazini mwa hifadhi ambao mahitaji yao wanayapata Arumeru na Arusha.

MAKAZI YA WAZUNGU

Ni ukweli usiopingika kuwa Meru imejazana na kubanana na Wazungu toka maeneo mbalimbali dunia. Ni kama historia mpya inayojirudia toka enzi za mababu zetu kuwa Meru ni sehemu mojawapo salama zaidi ya kuishi nchini Tanzania kutokana na hali yake ya hewa, mazingira mazuri pamoja na historia ya muda mrefu yenye mvuto.

• Kila siku nyuzi joto za eneo la Meru zinaanzia 21 – 27 c ambazo ni nyuzi joto nzuri zaidi kwa kuuwezesha mwili wa mwanadamu kufanya kazi bila tatizo. Hali hii iliifanya Meru kuwa sehemu muhimu ya makutano ya mambo mengi ya kiserikali hasa mikutano, semina na mafunzo mbalimbali.

• Ni sehemu yenye vivutio vya asili kama vile mila na desturi zinazokaribisha wageni bila ubaguzi.
• Ni sehemu iliyo salama zaidi kiafya bila kuwepo na magonjwa yaliyozoeleka kama yalivyo maeneo mengine yalivyo na malaria, homa za matumbo (typhoid) na mengine mengi.

• Ni sehemu kuu na muhimu ya vyanzo vya maji vinavyounda Mto Pangani kupitia Bonde la Mto Kikuletwa yaliko makutano ya mito na mifereji yote ya Meru.

• Ni Meru tu inayomiliki mlima wa pili kwa urefu Afrika ambapo hifadhi ya aina yake ina aina ya Kima wasiopatikana mahali pengine hapa nchini. Hifadhi hii kwa historia ilikuwa shamba la mifugo ya wakoloni na sehemu yake ilikuwa shamba la mapapai.

• Zaidi ya yote ni Meru iliyo na ardhi na maeneo tofauti unakoweza kulima zaidi ya aina kumi tofauti za mazao na kustawi bila tatizo.

Wenyewe wanasema, “Meru ni Nchi ya Ahadi kwa Wameru”.

1. SERENGETI NDOGO
Hapa ndiyo 'Serengeti Ndogo' ambako utakuta wanyama wengi.

Mtalii yeyote anaweza kushtuka wakati atakapoambiwa na Mhifadhi kwamba sasa anapelekwa katika Serengeti ndogo ndani ya Hifadhi ya Arusha. Eneo hilo siyo kubwa sana, lakini ni mbuga ya wazi inayofanana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Hapa wanyama mbalimbali wa mbuga za wazi wanaonekana kwa urahisi na kwa makundi, wakiwemo ngiri (warthog), pundamilia (zebra), kuro (waterbucks), twiga (giraffe) na mbogo (buffalo).  Nilimchekesha mhifadhi wakati nilipoona kundi na pundamilia wakiwa wamemzunguka mwenzao aliyelala chini ambaye nilidhani amekufa. “Ndugu, naona hawa wana msiba, mwenzao mmoja anaonekana kama amekufa!” Nikamwambia kwa mshtuko wakati nikipiga picha. Mhifadhi huyo akaniambia kwamba kwamba huyo hajafa, bali anajigalagaza. Kweli, dakika mbili baadaye nikamuona anagalagala.

“Kwa kawaida pundamilia huwa hawakusanyiki kwa msiba hata mwenzao anapokufa. Wanyama pekee ambao wanaweza kukusanyika kwa msiba ni tembo na nyani. Hata hivyo, nyani ndio wanaoongoza kwa kuomboleza msiba ambapo mwenzao akifa watambeba na kutembea naye kila waendako mpaka atakapooza na kunuka ndipo watamwacha. Lakini wanaomboleza kweli kama binadamu!” mhifadhi huyo akanieleza. Naam, tembea uone.

2. ‘OL DOINYO OROK’ NDIO MLIMA MERU
Oldoinyo Orok au Mlima Mweusi, ndio Mlima Meru


Jina la mlima huo limetokana na watu wa kabila la Wameru wanaoishi maeneo hayo yapata miaka 300 sasa. Kwa mujibu wa wanahistoria, eneo hili lilikuwa linakaliwa na Wamasai, ambao nao walikuwa wahamiaji. Wamasai wenyewe waliuita mlima huo Ol Doinyo Orok (yaani Mlima Mweusi) kama ilivyo kwa ile Milima ya Namanga ambayo mpaka sasa inaendelea kujulikana kwa jina hilo la Ol Doinyo Orok kule upande wa Kenya yenye urefu wa meta 2,548 (8,360 ft).

Mlima huo wa asili ya volcano ulioko takriban kilometa 70 magharibi mwa Mlima Kilimanjaro ni wa pili kwa urefu Tanzania ukiwa na urefu wa meta 4,565 (futi 14,977) kutoka usawa wa bahari na ni mlima wa tisa au wa kumi kwa urefu barani Afrika kati ya vilele 75 huku ukiwa wa 72 duniani. Mjerumani Fritz Jäger ndiye anayetajwa kuwa binadamu wa kwanza kufika kileleni mwaka 1904.

Kwa mujibu wa wanajiografia Siebert L, Simkin T (2002-), maeneo mengine ya volcano nchini Tanzania ni Mlima Kilimanjaro, Ol Doinyo Lengai ambao ni mlima pekee Afrika wenye volcano hai, Burko, Embulbul, Elan Nairobi, Esimingor, Gelai, Igwisi Hills, Izumbwe-Mpoli, Ketumbaine, Kieyo, Lemagrut, Loolmalasin, Ngorongoro, Ngozi, Oldeani, Ololmoti, Olossirwa, Mlima Rungwe na Bonde la Usangu.

Inaelezwa kwamba, Mlima Meru ndio ulikuwa mrefu zaidi kuliko Kilimanjaro, lakini ulipungua urefu kutokana na mlipuko wa volcano uliotokea takriban miaka 8,000 iliyopita ukaubomoa kama ilivyotokea kwa Mlima wa St. Helens huko Washington, Marekani mwaka 1980. Mlipuko huo uliufanya Mlima Meru uwe na umbo la nusu-duara, hivyo kufanya uwe sehemu ya maajabu kwa yeyote anayetembelea Hifadhi ya Arusha na kuupanda.

Mlipuko wa mwisho wa volcano ulitokea katika Mlima Meru mwaka 1910. Ukifika utastaajabu kuona vichuguu na kasoko ndogo ndogo zinazothibitisha kwamba kulikuwa na milipuko ya mara kwa mara ya volcano, ambayo ilisababisha sehemu kubwa ya udongo utiririke hadi katika maeneo ya West Kilimanjaro na Arusha Chini.

Mlima Meru ndio kiini cha Hifadhi ya Taifa ya Arusha, miteremko yake imetandwa na misitu minene ya savanna iliyohifadhi aina mbalimbali ya wanyama, zikiwemo aina 400 za ndege.
Unaweza kuupanda Mlima Meru kwa siku nne kwa kutumia mojawapo ya njia mbili zilizopo kutokea Lango la Momella (meta 1,500 kutoka usawa wa bahari). Unaweza kutumia njia ya Kaskazini ama Kusini na kufika kwenye mabanda ya Miriakamba kabla ya kuendelea na safari katika vituo vya Saddle hadi kileleni.

3. KASOKO YA NGURDOTO

Ngurdoto ni matokeo ya Wazungu kushindwa kutamka neno la Kimasai la Engur toto, yaani bonde katika mlima au kasoko (crater). Eneo hili la kasoko lipo katika Mlima Ngurdoto ambapo lina ukubwa wa kilometa za mraba 8 na mzingo wa kilometa 10.67 huku kina chake kikiwa cha meta 333.

Ukiwa katika eneo lenye mwinuko wa juu kabisa kwenye ukingo wa kasoko panapoitwa Leitong unakuwa kwenye kilele cha meta 1,824 kutoka usawa wa bahari. Tofauti na Kasoko ya Ngorongoro (Ngorongoro Crater), kwenye Kasoko ya Ngurdoto huwezi kushuka chini kutazama wanyama na mandhari, ingawa wapo wengi kama nyati wanaoonekana kwa makundi. Zamani walikuwepo faru wengi, lakini majambazi wakawapopoa na kuchukua vipusa.

Katika eneo hilo la Leitong unaweza kuiona hata barafu ya Mlima Kilimanjaro, maziwa ya Momella pamoja na kuona shughuli nyingi za kijamii, hasa kilimo, katika vijiji mbalimbali. Unyevu na ukungu mwingi kwenye eneo hili umesaidia kustawi kwa mimea aina mbalimbali kama feni, kuvumwani, okidi na kuvu (kuvumwani yenye vinyweleo).
Ni mahali pazuri kutembelea na panawavutia watalii wengi.

4. MSITU WA ASILI WA NGURDOTO
Mnyama jamii ya Mbega ndiyo alama ya Hifadhi hii na wanapatikana kwa wingi

Kama unataka hewa nzuri, ya asili na iliyotulia, basi tembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha, na ufike kwenye msitu huu wa asili wa Ngurdoto. Mandhari tulivu ya eneo hili yenye upepo mwanana usio na uchafuzi wowote wa mazingira utakusahaulisha msongo wa mawazo na mambo mengi ya kidunia. Kuna miti mingi aina kwa aina, ambayo imebandikwa vibao vyenye majina.

Msitu huu ndio pekee ambapo wanyama aina ya Mbega weupe wanapatikana kwa wingi katika Tanzania. Umekwishawahi kusikia usemi kwamba 'Mbega aliponzwa na uzuri wake?'. Basi uzuri wa wanyama hao ni wa pekee. Manyoya yao yanapendeza mno, halafu zile nyusi zao za asili hakika hata mwanamke ajipambe na atinde nyusi kiasi gani katu hawezi kuwafikia. Habari ndiyo hiyo!

Ni hifadhi chache sana pamoja na misitu ambamo Mbega wanapatikana. Lakini ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha ndimo wanamopatikana kwa wingi mno. Ni wanyama adimu na adhimu.

Mbega weupe-na-weusi ni ngedere wa kale wanaotokea katika jenasi ya Colobus, wakiwa wanapatikana zaidi barani Afrika. Wana uhusiano wa karibu na mbega wekundu wanaotokea kwenye jenasi ya Piliocolobus. Mbega ni jamii ya wanyama wasiokula nyama (herbivorous), chakula chao kikuu ni majani, matunda, maua na kadhalika. Yaani hawa jamaa ni ma-vegetarian hasa. Wanaishi katika makundi ya wanyama 9, kutegemeana na dume mmoja katika kundi la majike wengi na watoto.

Mbega ni muhimu kwa usambazaji wa mbegu kutokana na tabia yao ya ulaji na mfumo wa mmeng'enyo. Kuna aina tano ya spishi za kima hawa, huku kukiwa na spishi ndogo nane ambazo ni: Black colobus (C. satanas), Gabon black colobus (C. s. anthracinus), Bioko black colobus (C. s. satanas), Angola colobus (C. angolensis), Sclater’s Angola colobus (C. a. angolensis), Powell-Cotton’s Angola colobus (C. a. cottoni), Adolf Friedrichs’s Angola colobus au Ruwenzori black-and-white colobus (C. a. ruwenzorii), Cordier’s Angola colobus (C. a. cordieri), Prigogine's Angola colobus (C. a. prigoginei), Peters's Angola colobus au Tanzanian black-and-white colobus (C. a. palliatus), King colobus (C. polykomos), Ursine colobus (C. vellerosus) na Mantled guereza au Abyssinian black-and-white colobus (C. guereza).
Wanatokea katika Himaya ya Animalia, Faila ya Chordata, Daraja ya Mammalia, Oda ya Primates, Familia ya Cercopithecidae na Familia ndogo ya Colobinae.

5. MAZIWA YA MOMELLA

Ndege aina ya Flamingo wanavyoonekana katika Ziwa Momella Kubwa.

Haya ni maajabu mengine ambayo mtalii yeyote hapaswi kuyakosa. Maziwa haya ambayo maji yake yana magadi (alkaline) kwa miaka mingi yamekuwa mahali pa ndege kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni kuja kustarehe. Flamingo na Heroe kwa aina zake, wakiwemo wale wa Ziwa Natron (Ziwa Magadi), hujazana hapo wakipumzika kabla ya kurejea kwenye makazi yao ya asili.

Inaelezwa kwamba, ndege hao hutaga mayai huko Ziwa Natron na kuyaangua, ambapo baada ya muda huelekea kwenye maziwa haya ya Momella kujipumzisha kutokana na mazingira yake tulivu. Ukifika nyakati za asubuhi na jioni utashangaa kuona, hasa kwenye Ziwa Momella Kubwa, Flamingo wakiwa wametanda kama maua pembezoni mwa maziwa hayo na wengine wakiwa katikati na kutengeneza kundi linaloonekana kama kisiwa.

Maajabu ya maziwa haya ni kwamba, hakuna mito rasmi inayopeleka maji wala kutoa maji, isipokuwa inaelezwa kuwa yanapokea maji hayo kupitia kwenye mito inayopita chini ya ardhi. Maziwa hayo hayana kina kirefu, lakini pamoja na maji kuwa na chumvichumvi, yamekuwa matumizi muhimu kwa wanyama.

Ziwa Momella ndogo ndilo pekee ambapo wanyama aina ya Viboko hupatikana kutokana na maji yake kuwa na alkaline kidogo, lakini pia ndilo linalotumiwa kwa utalii wa makasia.

6. ZIWA LA IONGILI
Hili ndilo ziwa pekee miongoni mwa maziwa madogo matano yanayopatikana hifadhini ambalo maji yake hayana chumvi ambapo samaki aina ya perege (tilapia) wanapatikana. Ukiwa kwenye eneo hili utawaona wanyama kama viboko, mbogo na kuro huku mimea aina ya matete (mace) na mafunjo (papyrus) ikiwa inaonekana kama visiwa na huhama kulingana na mwelekeo wa upepo.

Hapa wanapatikana ndege wengi kama red knobbed coot, Africana, fish eagle na Africana jacana.

7. MAPOROMOKO YA MAJI

Ndani ya Hifadhi ya Arusha kuna maporomoko ya maji ya aina mbili – yale ya Tululusia na Maio, ambapo yanavutia sana kwa uzuri wake. Maporomoko ya Tululusia yana urefu wa meta 28 ambapo yapo karibu na Lango la Momella, wakati yale ya Maio yapo pembezoni mwa barabara iendayo mlimani.

Kabla ya kuyafikia maporomoko ya Tululusia kwa kupitia Njia ya Kaskazini ukiwa unapandisha Mlima Meru, lazima kwanza utakuwa umepata bahati ya kupita kwenye uwanda wa wazi ambapo utapata fursa ya kupiga picha kwa karibu na wanyama kama twiga na mbogo.
Kimsingi, eneo hili ndilo pekee ambalo unaweza kutembea na kuwakaribia wanyama hao, hasa mbogo, ukapiga nao picha kana kwamba unawachunga ng’ombe pori. Ni uzoefu unaokuja mara moja katika maisha na kwa hakika hutaweza kujutia safari yako.

8. TAO LA MTI
Hili ndilo Tao la Mti
Ukiwa na gari kama unakwenda Mlima Meru lazima upite kandokando ya mlima Tululusia ambao una mandhari nzuri ya kuvutia. Lakini baada ya kuupita mlima huo utakutana na kivutio kingine cha ajabu ambacho ni Tao la Mti wa Mkuyu (Fig Tree Arch).

Inaelezwa kwamba, mti huo uliota baada ya ndege wala matunda kudondosha punje za mkuyu kwenye mti mwingine wa asili, ambapo baadaye mkuyu ukaota kama tao, ambalo ni kubwa kiasi kwamba gari lenye ukubwa wa tembo linaweza kupita bila shida.

Hiki ni kivutio kingine ambacho hakika unapaswa kukitembelea na kujionea maajabu haya na hasa kwa Mti wa Mkuyu ambao una maajabu yake. Kama ulikuwa hujui,  Mkuyu ndiye malkia wa miti yote ulimwenguni na kuna watu wanaouita mti mtakatifu. Wacha nikuelezee kidogo kuhusu mti huo:

Nakumbuka enzi za utotoni tulizowea kuambiwa mti wa mbuyu ni wa mashetani na tusithubutu hata siku moja kukaa karibu pindi mvua inaponyesha kwa sababu radi linaweza kuupiga na kuugawanya katikati. Hata hivyo, bado tuliendelea kukwea na kuchuma matunda yake nyakati za kiangazi.

Tuliambiwa kwamba wachawi hupendelea kuweka maskani yao kwenye miti hiyo ya mibuyu, ambayo ni miongoni mwa miti mikubwa na inayoweza kukua na kumea katika maeneo yenye ukame, kama Dodoma na Singida kwa hapa Tanzania.

Lakini ukiachilia mbali mbuyu, pia wazee wetu walikuwa wakitukataza tusipendelee kucheza kwenye miti ya mikuyu, ambayo inatajwa kwamba ndiyo ‘malkia wa miti yote’. Sababu kubwa waliyotuambia ni kwamba miti hiyo ni ya miungu na ndiyo maana inapendelea kuota sehemu zilizotulia kwenye mapito ya maji huku ikiwa inaongoza kwa kuwa miti pekee yenye mizizi mingi.

“Ninyi hamuoni, hata nyakati za kiangazi mti unaonekana umependeza, tofauti na ule mbuyu. Ule mbuyu ni mti wa mashetani, lakini huu ni mti wa miungu. Msije mkathubutu hata siku moja kuukata ama kuuchezea, miungu ikikasirika mtapata shida,” nakumbuka mzee mmoja alipata kutuambia wakati tukiwa wadogo.

Kweli hatukuwa tukiikata miti hiyo, lakini daima tulipendelea kucheza chini ya vivuli vyake na kukwea kuchuma matunda yake mazuri kuyatazama, matamu kuyala, lakini yakiwa yamejaa wadudu wengi ambao unalazimika kuwaondoa kabla ya kuyala.

Huo ndio mkuyu, mti ambao ni wa ajabu ambao si wengi wanaoufahamu kutokana na kutoota kila mahali kama ilivyo miti mingine. Tena basi si mti wa kupandwa, bali hujiotea wenyewe, hasa katika maeneo ya kitropiki, ingawa baadhi ya jamii yake inaweza kuota kwenye maeneo ya joto.

Tunaambiwa kwamba mti mashuhuri wa mkuyu (Ficus carica) asili yake ni Asia na Mashariki ya Kati lakini umefanikiwa kumea hata katika maeneo mengine, ukiwa unazaa matunda matamu sana, ambayo kama unaweza kuhudumiwa kama yalivyo matunda mengine, huwezi kukuta wadudu ndani ya matunda yake yenye majimaji mengi.

Wataalamu wa mambo ya kale wanasema kwamba mti huu wa mkuyu unaweza kuwa mmoja kati ya mimea iliyowahi kutunzwa na binadamu (katika sehemu nyingine mikuyu inatunzwa, hasa kwa watu wenye maeneo makubwa, kwa sababu miti hii huchukua maeneo makubwa sana kutokana na mfumo wao wa mizizi kuwa yenye kutambaa). Mkuyu unatajwa ndani ya Biblia, wakati Adam na Eva wanapotumia majani yake kujistiri baada ya kuona wako uchi ndani ya Bustani ya Eden.

Ukristo siyo dini pekee ambayo imeupa mkuyu nafasi kubwa kama unavyotajwa pia katika Injili. Jamii nyingine ya mkuyu au mtini wa Kiasia, Ficus religiosa, unachukuliwa kama mti mtakatifu na Wahindu, Wajaini, na Mabuddha. Inasemekana Buddha Mkuu, Siddhartha Gautama, alipata ufunuo wakati alipokuwa ameketi chini ya mti mtakatifu wa mkuyu, ambao pia unajulikana kama bo au pipal. Waislamu pia wanaichukulia miti mingine ya jamii ya mkuyu kama mitakatifu.

Kwa hakika, kati ya miti yote duniani, mikuyu (Ficus) ndiyo miti pekee ambayo ukuaji wake umetandwa na utata utata na hata uchavushaji wake ni wa ajabu. Jaribu kufikiria mti ukiwa umejaa mizizi inayofanana na nyoka, ikiwa imejiviringisha na kuchomoza kwenye shina ama matawi ya mti mkubwa na kutanda kila sehemu na hata kuinyonga miti mingine ya jirani yake.

Miti hii ambayo iko katika jenasi ya Ficus, katika familia ya Mulberry (Moraceae), ndiyo yenye jamii kubwa zaidi ikiwa na aina ya miti 1,000. Miti inayoifuatia kwa kuwa na jamii nyingi ni ile ya jamii ya mikungugu yenye miiba, maarufu kama Acacia (ambayo ina jamii 800), Mikaratusi ama Eucalyptus (500), na Cassia (500).

Wazee wetu walikuwa na akili sana – japo hawakuwa na elimu ya darasani – lakini walijua namna ya kutunza mazingira. Walitukataza tusiiharibu miti hiyo kwani mara nyingi huota katika vyanzo vya maji au sehemu iliyopitisha maji kama mto, au sehemu iliyokuwa na uoto mzuri na ardhi yenye rutuba.

Kama iliota sehemu za nyikani, basi tuliamini kwamba ikiwa utachimba kisima mahali hapo maji hayakuwa mbali sana, na ndivyo ilivyokuwa, hasa kwa sisi ambao tulikuwa tukiishi katika maeneo kame kama yale ya mikoa ya kati.
Faida yake ni kubwa, kwamba pamoja na kuwa vyanzo vya maji na vivutio vya mawingu ya mvua, lakini matunda yake ni chakula kizuri sana kwa ndege, wanyama wa porini na hata binadamu.

Tunaambiwa kwamba matunda ya mkuyu yana viiniisho kama wanga, hamirojo, sukari, mafuta na protini kibao, hivyo ni mazuri sana kuliwa. Kwa sisi tuliowahi kuyala wakati wa utotoni tunaujua utamu wake, lakini linaweza kuwa jambo geni kwa wale ambao hata mti wenyewe hawaujui.

Tunda la mkuyu linachukuliwa kama tunda, lakini kwa hakika hilo ndilo kama ua la mkuyu. Linaweza kutajwa kama ni tunda bandia ama tunda linalojipogolesha, ambapo ua na mbegu hukua pamoja na kufanya tunda.

Pengine uwezo huu wa kutoa maua ambayo ni matunda, tofauti na miti mingine, ndiyo yaliyowafanya hata wazee wetu waone kwamba huu ulikuwa ni mti wa miungu, tofauti na mbuyu ambao maua yake yanaonekana mpaka matunda yanapokomaa.

Maelezo mengine watakupatia wahifadhi na watalaamu wa mimea mara utakapofika kwenye hifadhi hii, mimi nimekupatia uzoefu wangu tu wa uhifadhi wa asili.

9. KASOKO YA MERU

Kila eneo lina raha yake kulitazama. Ukiwa unapanda Mlima Meru lazima utapita kwenye uwanda wa wazi ambao unajulikana zaidi kama Mandhari ya Kitoto, ambapo unaweza kuona mazingira ya Momella, pori la wazi na Mlima Kilimanjaro.

Lakini ukipita eneo hilo utakuta kuna njia nyembamba ambayo inaishia kwenye Kasoko ya Meru. Hapo utaona kitu kilichosimama kama ukucha wa ndege wa kuparura ndani ya kasoko, ambako kwa uhakika ni majivu ya volcano yenye umbo kama pia.

Kasoko ya Meru ni eneo tambarare na lenye kuvutia ambapo unaweza kuona vizuri mofolojia yam lima hasa siku zisizo na mawingu.

10. TAMBIKO LA WAMERU

Njia nyembamba inayoanzia kasoko ya Meru huelekea kwenye mandhari ya Njeku kupitia mandhari nzuri ya Ash-cone na kasoko, ambapo kuna jukwaa kwenye mwinuko wa juu unaotazamana na maporomoko ya maji katika korongo la mto wa Ngarenanyuki.

Wakati wa ukame Wameru hulitumia eneo hilo kutambikia mungu wao chini ya mti ujulikanao kama African pencial cidar (Juniper) ambao upo karibu na tambarare ya kasoko. Kadiri miaka inavyozidi kusonga mbele, matambiko haya yanaelekea kupungua hifadhini, lakini eneo hili bado limekuwa kivutio kikubwa kwa watalii.

WANYAMA NA NDEGE
Huyu ni Hondohondo wa jamii ya Decken Toko Tockus deckeni

Pamoja na kuwa na eneo dogo la hifadhi, lakini hifadhi hii ina utajiri mkubwa wa wanyama kama twiga, pundamilia, mbogo, ngiri, mbega, kima, tembo, chui. Hakuna simba kwenye hifadhi hiyo.

Utajiri mkubwa ulioko humo ni ndege aina kwa aina, ambapo miongoni mwao ni Korongo, Njiwa, Kunguru, Tai, Kipanga, Yangeyange, Kibisi, Shakwe, Dudumizi, Firigogo, Kasuku, Shorobo, Kekeo, Mdiria, Hondohondo, Zuwakulu, Kigong'ota, Shore, Kuzi au Kwenzi kwa jamii zake na kadhalika

No comments:

Post a Comment