Afisa Usalama wa Chakula (TBS), Elisha Meshack akikagua bidhaa mbalimbali katika maduka yaliyopo Kasulu mkoani Kigoma ili kuhakiki ubora wa bidhaa hizo.

********************************

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea na mpango wa ukaguzi wa kushtukiza sokoni kwa wasambazaji na wauzaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo za chakula katika wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Ukaguzi huu umelenga kuhakiki iwapo bidhaa zinazouzwa sokoni zimekidhi ubora kwa kufuata matakwa ya kiwango husika na vilevile kuhakikisha bidhaa zote zilizopo sokoni zinafaa kwa matumizi ya binadamu ikiwemo kuhakiki muda wa matumizi wa bidhaa hizo.

Ukaguzi huo ulienda sambamba na utoaji elimu kwa wauzaji na wanunuaji juu ya uhifadhi sahihi wa bidhaa na umuhimu wa kuzingatia na kusoma taarifa sahihi na muhimu katika vifungashio.

Kwa upande wake Afisa Usalama wa Chakula (TBS), Elisha Meshack ametoa wito kwa waingizaji na wauzaji wa bidhaa zilizo katika viwango vya lazima kuzingatia sheria na taratibu za uingizaji na uuzaji bidhaa kwa kuuza na kuingiza bidhaa ambazo ni bora na salama ili kukuza biashara na kuepuka kupoteza masoko na kero ya kukutwa na bidhaa hafifu ambayo itawalazimu kuziteketeza kwa gharama zao.

Pia aliwashauri wasisite kuwasiliana na ofisi ya TBS mara kwa mara pale wanapohitaji msaada wa kitaalamu.

“Ukaguzi huu ni iendelevu kwani ni moja ya majukumu ya Shirika na utahusisha bidhaa mbalimbali ambapo lengo ni kuhakikisha wananchi wanatumia bidhaa zenye ubora kwa ajili ya kulinda mazingira na afya zao” alisema Meshack.

Vilevile alisema katika ukaguzi huu TBS inakagua maduka ya chakula na vipodozi ambayo hayajasajiliwa na hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa kwa wale ambao watabainika bado hawajafanya mchakato wa kusajili maduka hayo.

Ukaguzi huu unatarajiwa kufanyika katika wilaya zingine pia za mkoa wa Kigoma ikiwemo Kibondo na Kakonko na katika mikoa mingine inayohusisha kanda ya Magharibi ambayo ni Katavi na Rukwa.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: