Tuesday, 24 August 2021

Tozo ya Majengo kupitia Luku yapokelewa Manyara

 Na John Walter-Manyara
MAMLAKA ya Mapato Tanzania(TRA) imetolea ufafanuzi masuala mbalimbali yahusuyo kodi hiyo ya majengo ikiwamo mkanganyiko kuhusu ulipaji wa kodi hiyo kwenye nyumba zenye hadhi tofauti, nyumba zilizoezekwa kwa nyasi hazihusiki kwenye tozo hiyo.

TRA wametoa ufafanuzi kwenye mjadala na wafanyabiashara katika mji wa Babati kuhusu ulipaji kodi ya majengo kwa njia ya ‘luku’ ya umeme uliofanyika katika ukumbi wa River Nile mjini Babati.

Afisa Elimu na huduma kwa mlipakodi kutoka TRA makao makuu Lazaro Mafie, alisema utaratibu wa kulipia kodi ya majengo kwa njia ya mfumo wa luku umeanza Agosti 20,2021 na utakuwa ukitekelezwa kwa njia hiyo ukimhusu mwenye nyumba na sio mpangaji.

Amesema tozo hiyo inatozwa mara moja katika mwezi kwa maana mteja akishalipa hata umeme unapoisha katikati, hatakatwa tena hadi mwezi mwingine.

Kwa makato hayo inamaanisha kwamba kwa kipindi cha mwaka mmoja mlipaji atakuwa anatozwa Sh 12,000 ambayo ndiyo kodi ya jengo kwa nyumba za kawaida.

Aidha Mafie amesema Kodi hiyo haihusu nyumba za vijijini, nyumba za nyasi na udongo na zile zilizojengwa kwa vifaa visivyodumu.

Amesema jengo la ghorofa lililo kwenye mji, manispaa na jiji, kila sakafu inatozwa kwa mwezi kwenye luku Sh 5,000 ili ndani ya mwaka mlipaji awe amelipa Sh 60,000 ambayo ndicho kiwango cha kodi kwa nyumba ya mtindo huo.

Aidha nyumba ya ghorofa zilizopo wilayani, halmashauri na mikoani zitalipa Sh 12,000 kama nyumba za kawaida bila kuja idadi ya sakafu zilizopo katika jengo hilo la ghorofa.

Alisema wastaafu, wazee wenye umri kuanzia miaka 60 na kuendelea wako kwenye kundi la msamaha na wataendelea kupata msamaha huo wa kodi ya majengo kwenye nyumba za makazi wanayoishi wenyewe.

Alisema utaratibu wa kupata msamaha bado unaendelea na ni wa mtu yeyote aliyekidhi vigezo vya msamaha wa kodi ya majengo kwa mujibu wa sheria,nyumba za ibada na nyumba za serikali.

Aidha amewataka wateja waliokatwa kimakosa kwenye luku watoe taarifa ofisi za TRA akiwa na nyaraka na kiasi kilichokatwa kitaingizwa kwenye umeme wa luku yake.

Kwa upande wa nyumba zisizo na umeme ambazo zipo kwenye kundi la kulipa kodi, zinapaswa kulipa na mmiliki ana wajibu wa kufuata ankara ya malipo TRA.

Kuhusu nyumba moja yenye mita zaidi ya moja, Mafie alieleza kuwa kodi hiyo italipiwa kupitia luku moja na ikiwa mteja ametozwa kwenye mita zaidi ya moja atapaswa kuwasilisha taarifa TRA ili makato yaelekezwe kwenye moja.

Kuhusu kiwanja kimoja kuwa na nyumba zaidi ya moja, alisema kila nyumba inapaswa kulipiwa kodi ya jengo.

Kaimu Meneja wa TRA mkoa wa Manyara amesema wataendelea kuwaelimisha wateja wao kuhusu sheria hiyo huku akiwahimiza kulipa kodi zao kwa wakati na kwa usahihi pamoja na kutumia mashine za kielektroniki wakati wote kama sheria inavyowataka.

Mfanyabiashara kutoka mjini Babati Isack Mushi (POLEPOLE) ameunga mkono utaratibu huo wa Serikali na kushauri elimu Zaidi iendelee kutolewa kwa wananchi.

Hivi karibuni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lilielekeza wanaotaka kununua umeme kuanzia mwezi Agosti wahakikishe wananunua wa zaidi ya Sh 2,000 waweze kulipa kodi ya majengo ambayo imeanza kukatwa kupitia mfumo wa luku za umeme.

No comments:

Post a Comment