Na WAMJW - Katavi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Afya kurejesha usimamizi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi kwa Katibu Tawala Mkoa wa Katavi.

Mhe. Kassim Majaliwa amesema hayo mara baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa jengo la Hospitali hiyo Katika Manispaa ya Mpanda na kuonyesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi.

“Moja ya malengo ya ziara yangu ni kuja kuona ujenzi wa jengo hili, ujenzi wa jengo hili umesuasua sana, haujaniridhisha” amesema Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa

Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi umeanza toka mwaka 2018 huku hadi kufikia mwezi huu hatua za ujenzi zimefikia asilimia 45 na kuleta sintofahamu kwa wananchi katika uhakika wa upatikanaji wa huduma bora za matibabu ya rufaa jirani na makazi yao.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Kassim Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel kurejesha haraka usimamizi wa ujenzi wa Hospitali hiyo kwa Katibu Tawala Mkoa wa Katavi ili wawe wasimamizi wakuu na karibu katika mradi huo.

“Kama Mikoa mingine tumetumia Makatibu Tawala kujenga, nyie mlimpa Katibu Tawala Mkoa kujenga, mkarudisha Wizarani ambapo wataalam mpo Dodoma, jengo liko Katavi, mtaweza kweli kusimamia ujenzi?” amehoji Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan imejipanga kusogeza karibu huduma za matibabu kwa wananchi na tayari Mheshimiwa Rais ametoa kiasi cha Shilingi Milioni 688 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali hiyo.

Mhe. Kassim amemuagiza Katibu Tawala Mkoa wa Katavi kuunda kamati ya usimamizi wa ujenzi wa Hospitali hiyo na kuitambulisha kwa viongozi ndani ya Mkoa huo ili nao waweze kusimamia kwa ukaribu hatua za ujenzi wa Hosptali hiyo huku akiwaonya kutumia vyema fedha hizo ili kuweza kukamilisha upande mmoja wa jengo hilo ili huduma zianze kutolewa kwa wananchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Wizara imeyapokea na kuanza utekelezaji wa mara moja kuhakikisha fedha zilizotolewa zinasimamiwa na Katibu Tawala Mkoa wa Katavi.

Dkt. Mollel amesema kuwa kwa kipindi kilichobaki cha miezi 10 Wizara itahakikisha inashirikiana kwa ukaribu zaidi na Uongozi wa Mkoa wa Katavi ili kuweza kukamilisha lengo kusudiwa na huduma za matibabu zianze kutolewa kwa wananchi.

Awali akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba Dkt. Caroline Mayengo amesema kuwa ujenzi wa Hospitali hiyo unatarajia kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 12.2 chini ya uratibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mkandarasi SUMA JKT na Mshauri Elekezi Crystal Consultants.

Dkt. Caroline amesema kuwa ujenzi wa Hospitali hiyo unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huu ilianza na majengo mawili ambayo ni jengo kuu lenye ghorofa moja lenye Kitalu A na B litakalotoa huduma za afya ya uzazi mama na mtoto (Maternity), huduma za dharura (EMD), wagonjwa wa Nje (OPD), Famasi, huduma za Radiolojia, Huduma za upasuaji na huduma za uangalizi Maalumu (ICU) pamoja na jengo la Maabara.




Share To:

Post A Comment: