Sunday, 1 August 2021

MBUNGE MLIMBA AKAMILISHA UJENZI WA DARASA SHULE YA SEKONDARI LONDO

 

Mmoja wa wanafunzi wa Sekondari ya Londo Kata ya Mbingu Jimbo la Mlimba akimshukuru Mbunge wa Jimbo hilo, Godwin Kunambi la kufanikisha ujenzi wa Darasa katika Shule hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Londo alipowatembelea kujionea ukamilikaji wa Darasa Moja ambalo amefanikisha ujenzi wake, Darasa hilo limegharimu Sh Milioni 10.
Mbunge wa Jimbo la Mlimba Godwin Kunambi akitoka kukagua Darasa ambalo amefanikisha ujenzi wake katika Shule ya Sekondari Londo iliyopo Kata ya Mbingu. Ujenzi wa Darasa hili umegharimu Sh Milioni 10.
Hongera sana! Mmoja wa wazee katika Kata ya Mbingu akimshukuru Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi kwa kufanya ujenzi wa Darasa katika Shule ya Sekondari Londo.

Charles James,

AMETEKELEZA! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mbunge wa Jimbo la Mlimba Morogoro, Godwin Kunambi kukabidhi chumba kimoja cha Darasa kwenye Shule ya Sekondari ya Londo iliyopo Kata ya Mbingu jimboni humo.

Ujenzi wa Darasa hilo umetokana na ahadi ya Mbunge Kunambi alipofanya ziara ya kusikiliza changamoto za wananchi wa kata hiyo ambapo alikutana na changamoto katika Shule hiyo ambapo aliahidi kufanikisha ujenzi wake pamoja kuwasilisha changamoto ya uhaba wa walimu.

Katika ajira mpya za walimu zilizotolewa na Serikali, Shule hiyo ya Londo imepata walimu watatu ambao wamepunguza uhaba wa walimu jambo ambalo Mbunge Kunambi aliahidi kulishughulikia pia katika ziara yake ya mwezi Februari.

Akizungumza baada ya kufika katika Shule hiyo, Kunambi amesema baada ya kukamilika kwa Darasa hilo na kupatikana kwa Walimu watatu ni wajibu wake na wananchi kushirikiana katika kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Walimu ambayo ni changamoto shuleni hapo.

" Ni jambo la faraja kuona tumekamilisha ujenzi wa Darasa hili ambalo limegharimu Sh Milioni 10, niishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuwezesha pia kutupatia Walimu watatu na hivyo kuondoa changamoto ya uhaba wa walimu iliyokua ikitukabili.

Ni wazi sasa tunapaswa kuhakikisha tunahamishia Nguvu zetu katika kuinua elimu katika Shule yetu ya Londo na Jimbo letu kwa ujumla, tujenge miundombinu bora kwa wanafunzi wetu ambayo itasaidia kukuza ufaulu wao," Amesema Kunambi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo, Nestor Kyelula amempongeza Mbunge Kunambi kwa kufanikisha ujenzi wa Darasa hilo huku akimuahidi kuendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo waliinadi pamoja.

" Kwa kweli umetushika mkono kwa kiwango kikubwa Mhe Mbunge, tulikua na uhaba wa madarasa lakini kupata Darasa hili kwetu ni mchango mkubwa, tukuhakikishie Kupambana kwa pamoja na Walimu wetu katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi wetu," Amesema Kyelula.

Nae mmoja wa Wanafunzi wa kidato cha pili shuleni hapo amemshukuru Mbunge huyo kwa mchango wake akisema umeweka alama mioyoni mwao na kuongeza ari ya kusoma kwa bidii ili na wao waje kuwa viongozi watakaosaidia Jimbo la Mlimba.

No comments:

Post a Comment