Tuesday, 10 August 2021

MAAFISA FORODHA MIPAKANI WASISITIZWA KUHUSU MATUMIZI SAHIHI YA SHERIA ZA OSBP ILI KUHAMASISHA WATUMIAJI

 Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Msafiri Mbibo akiongea na Watumishi wa TRA pamoja na watumishi wengine wa baadhi ya taasisi za Serikali zinazofanya kazi pamoja katika Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Mutukula mkoani Kagera ambapo ni mpakani mwa Tanzania na Uganda, kuhusu namna ya kushirikiana kwa pamoja na kuwa na nidhamu katika kazi zao wanapokua mpakani hapo.

Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Msafiri Mbibo (wa pili kulia) akiongea na kutoa maagizo mbalimbali kwa viongozi wa TRA katika ofisi ya TRA iliyopo eneo la Kyaka mkoani Kagera wakati alipofanya ziara yake ya kikazi mkoani hapo kwa ajili ya kusikiliza changamoto mbalimbali katika mpaka wa Tanzania na Uganda.Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Msafiri Mbibo akimsikiliza Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Profesa Faustin Kamuzora (kushoto) wakati alipomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kufanya nae mazungumzo juu ya masuala mbalimbali ya kodi ikiwemo namna bora ya kuboresha makusanyo ya mapato ya Serikali.

PICHA ZOTE NA TRA

………………………………………………………………

Na. Mwandishi wetu

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imewataka Maafisa Forodha wa TRA pamoja na maafisa wa taasisi nyingine za Serikali kuhakikisha kuwa wanahamasisha matumizi sahihi ya kisheria katika Vituo vya Huduma kwa Pamoja Mpakani ili watu mbalimbali wanaopita kupitia katika mipaka hiyo waweze kuhamasika kutumia njia sahihi badala ya njia zisizo rasmi.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Naibu Kamishna wa TRA, Bw. Msafiri Mbibo wakati alipofanya ziara yake ya kikazi katika mpaka wa Mutukula unaounganisha nchi ya Tanzania na Uganda uliopo mkoani Kagera.

Bwana Mbibo amesema kwamba, lengo la kutaka kuwepo kwa matumizi sahihi ya sheria hizo katika maeneo ya mipakani ni kuzuia watumiaji kutumia njia zisizo rasmi ambazo zinaweza kuathiri takwimu za kiuchumi, kuhatarisha usalama wa nchi na pia uingizaji bidhaa mbazo hazina viwango ambazo zitaumiza walaji wa ndani na zinaweza kuharibu mahusiano baina ya Tanzania na nchi za jirani.

“Kuziingiza bidhaa ambazo hazina viwango nchini kwetu na kupeleka bidhaa ambazo hazina viwango kwa nchi ambazo ni majirani zetu kutaharibu mahusiano yetu ya kibiashara pindi wakigundua tunaingiza nchini mwao bidhaa za namna hiyo, hivyo lazima tusimamie vizuri sheria ili mambo haya yasitokee”, alisema Mbibo.

Ameongeza kuwa, mpaka wa Mutukula kwa sasa ufanisi wake unaoongezeka mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2020/2021 ulipangiwa lengo la kukusanya shilingi bilioni 21 na umefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 24 ambapo hiyo ni sawa ufanisi wa utendaji wa asilimia 114 ikilinganishwa na mwaka wa fedha wa 2019/2021 malengo yalikua ni kukusanya shilingi bilioni 18 na zikakusanywa shilingi bilioni 20 na zaidi.

“Mpaka huu ni wakutegemewa na unafanya vizuri zaidi, na endapo tutazidi kuongeza huduma au vitendea kazi katika mpaka huu basi ufanisi huu wa sasa utazidi kuongezeka na tutaweza kuwahudumia wananchi wa nchi jirani na Watanzania pia”

Aidha, amefafanua kuhusu magari yaliyopo mpakani hapo kwa kusema kwamba, baadhi ya magari ambayo hayajakamilisha baadhi ya taratibu ndogo ndogo wahusika huwa wanaitwa ili waweze kukamilisha taratibu hizo ili waweze kulipa kodi zao na kuyaondoa, lakini pia kwa wale ambao wameyatelekeza magari yao sheria inaitaka TRA kutangaza kwa muda fulani ili wahusika wenyewe wajitokeze na kukamilisha taratibu za kiforodha na endapo hawajafanya hivyo baada ya siku kadhaa kupita sheria inaitaka pia TRA iyaingize magari hayo katika mnada ambao mtu atayevutiwa nayo aweze kuyanunua ili kodi ya Serikali iweze kukombolewa.

“Mnada wa kuuza magari yaliyotelekezwa tunafanya kwa njia ya mtandao (Online), hivyo mtu yeyote nchi nzima anaweza kushiriki katika mnada, lakini kuna baadhi ya magari ya watu ambao ni wakorofi na wamekua wakichezea chesisi namba za magari na kwa bahati nzuri sheria inamruhusu Kamishna Mkuu wa TRA kuyatoa kwa namna anavyotaka yeye, basi sisi tunaweza kuyagawa kwa taasisi nyingine za Serikali lakini hii huwa hatufanyi mara kwa mara”, alisema Mbibo.

Naibu Kamishna Mkuu wa TRA yuko katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Kanda ya ziwa na lengo la ziara hiyo ni kuona namna ya utendaji kazi wa ofisi za TRA mipakani ikiwemo kusikiliza changamoto mbalimbali katika ofisi hizo ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi wake na hatimaye makusanyo ya mapato yazidi kuongezeka na kwenda kuleta maendeleo kwa Taifa.

No comments:

Post a Comment