Wednesday, 14 July 2021

Skimu ya Muungano Matufa-Mawemairo yapata viongozi wapya.

 


Na John Walter-Babati

Jumuiya ya Watumia Maji Skimu ya Muungano (WUA) Mawemairo-Matufa katika kata ya Magugu wilayani Babati mkoa wa Manyara, imepata viongozi wapya  baada ya kufanyika uchaguzi ambapo watahudumu katika nafasi zao kwa muda wa miaka mitatu.

Uchaguzi huo ulifanyika juzi eneo la Mpaka wa Mawemairo na Matufa nje kidogo ya Mji mdogo wa Magugu na kuhudhuriwa na watendaji wa kata na wenyeviti wa vijiji wanaotumia Skimu hiyo ambayo jumuiya hiyo itakuwa na jukumu la kulilinda.

Katika uchaguzi huo walipatikana wajumbe nane,wane kutoka kijiji cha Matufa na wengine wane kijiji cha Mawemairo ambao wameunda jumuiya hiyo kwa kuzingatia jinsia na makundi ya wafugaji, wakulima na watumiaji wa maji.

Baada ya wajumbe hao wa Bodi kupatikana watakutana siku ya ijumaa na kumchagua Mwenyekiti na makamu wake huku katibu akiajiriwa kwa mujibu wa katiba ya WUA.

Diwani wa kata ya Magugu Filbert Modemba amewataka wanajumuiya wautumie vizuri mradi huo ili uwe na tija  kwa maendeleo yao,Hlamashauri na Taifa kwa ujumla kwa kuwa umetumia gharama kubwa.

“Mimi kama diwani wenu nitakuwa bega kwa bega kuhakikisha kwamba mradi huu unakusanya mamilioni ya pesa ili mwisho wa siku utunufaishe hata mnapokutana kwenye vikao mnywe na kula kwa pesa zenu”alisema Modemba

Amewataka wanachama kuonyesha ushirikiano kwa viongozi waliochaguliwa ili waweze kufikia malengo ya kuifikisha jumuiya mbali Zaidi.

Afisa Umwagiliaji wilaya ya Babati Emmanuel Nyeku amesema Skimu ya Muungano yenye ukubwa wa hekari 1,623 ambapo  linazalishwa zao la Mpunga huku sehemu kubwa ikiwa ni Miwa kutokana na fursa zinazoonekana kwenye kiwanda cha Sukari Manyara Sugar kilichopo kwenye kata ya Magugu.

Akizungunza kwa niaba ya wenzake Juma Kawaka  alisema watashirikiana na wana jumuiya hiyo na kuhakikisha kila kilichokusudiwa kinakwenda sawa ikiwa ni pamoja na kulinda rasilimali za maji katika eneo hilo.

Amesema Skimu hiyo ni Tunu yao na ni haki yao kuilinda kwani imewatoa katika hali duni ya Maisha na kuwainua kwani wengi wao wameweza kujenga,kulea familia zao na hata kumiliki vyombo vya moto.

No comments:

Post a Comment