Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza kufanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Saalam, Julai 4,2021.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, watumishi wa Wizara na Taasisi zake, watumishi wa bandari,wakiwa katika ziara katika bandari ya Dar es Saalam, Julai 4,2021.



Transfoma ikiwa tayari imepakiwa kwenye gari kwaajili ya kupelekwa katika mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere(JNHPP).







Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,(kushoto) Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali(katikati) wakiwasili katika Bandari ya Dar es Salaam kwaajili ya ziara ya kushtukiza, Julai 4,2021.

………………………………………………………………………….

Hafsa Omar-Dar es Salaam

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amesema ifikapo tarehe 12 mwezi huu transfoma zote sita ambazo zipo Bandari ya Dar es Salaam ziwe zimeshasafirishwa kwenda kwenye ujenzi wa mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere(JNHPP).

Ameyasema hayo, 4 Julai, 2021 wakati wa ziara ya kushtukiza kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka.

Dkt. Kalemani,amesema amefanya ziara hiyo ili kujua sababu ambazo zimepelekea kucheleweshwa kwa kuondolewa kwa Transfoma hizo katika bandari hiyo, ambapo zinatakiwa kupelekwa katika mradi wa Julius Nyerere ili kuendelea na ujenzi wa mradi huo.

Ameeleza kuwa, mwezi uliopita alipotembelea mradi wa Julius Nyerere alihakikishiwa kuwa transfoma hizo zitafika kwa wakati katika mradi huo lakini mpaka sasa bado zipo bandarini.

“ hizi Transfoma zimekwamishwa na nini , kwanini zimalize mwezi mzima bandarini na wakati zilitakiwa ziwe zimetoka naomba niseme sitavumilia hii hali, huu mradi wenyewe ni wa haraka haraka kila mmoja anauhitaji kwahiyo hatutavumilia mtu yoyote atucheleweshe,”alisema.

Aidha, amewataka waatalamu wote ambao wanaohusika na nyaraka ambazo zinahusika na uletaji wa vifaa nchini, wakizipata nyaraka hizo waanze mara moja na taratibu zote za utoaji wa mizigo bandarini.

Pia, amewataka watumishi wa bandari kutoa ushirikiano kwa Wizara ili kuweza kutatua changamoto zozote ambazo zitajitokeza na kuwataka kuwasiliana na viongozi wa Wizara ili kumaliza changamoto hizo kwa haraka.

“hatutaki kuona vifaa vinavyokwenda kwenye miradi vinakaa bandarini mahala pake pa kukaa sio bandarini ni kwenye miradi na Mhe. Rais ametupa fedha tena za kutosha na mkandarasi hadai chochote kwahiyo hivi vifaa vinakiwa kuwa kwenye mradi ili mkandarasi aendelee na kazi,” alisisitiza Dkt. Kalemani.

Vilevile, amesema ataendelea kuwasiliana na watumishi wa bandari ili kuhakikisha kuwa transfoma ambayo ilipaswa kuondoka leo kwenda kwenye mradi inaondoka ili ifungwe na kuanza kufanya kazi.
Share To:

Post A Comment: