Meneja wa Mradi wa Mkuju Bwa. Beria Vorster akionyesha kifaa cha kupimia mionzi inayotoka katika madini ya ureniam kwa Bodi ya Wakurugenzi wa NEMC.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Muhandisi Dkt. Samuel Gwamaka, akielezea jambo wakati wa ukaguzi wa mradi wa Uraniam uliopo Namtumbo Mkoani Ruvuma.
Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), wakisikiliza maelezo yanayotolewa na Meneja wa Mradi wa uraniam wa Mkuju kutoka kampuni ya Mantra Tanzania Limited Bwa. Beria Vorster.

Na Mwandishi wetu
BODIya Wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC), imefanya ziara katika mradi wa kuchimba madini aina ya uraniam unaoendeshwa na kampuni ya Mantra Tanzania Limited, ambao unatarajia kuanza kuchimba hivi karibuni madini hayo yatatumika kwa ajili ya kuzalisha nishati ya umeme. Mradi uliopo maeneo ya Mkuju Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma.

Bodi hio imetembelea mradi huo ili kukagua na kujiridhisha kuhusu hali ya kimazingira ili mradi utakapoanza usiwe na athari kimazingira na kijamii bali uwe chachu ya maendeleo katika Taifa letu.

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Muhandisi Dkt.Samuel Gwamaka amesema kuwa, watu wengi katika jamii yetu wamekuwa na uelewa mdogo juu ya madini haya aina ya uraniam kwani wanaamini kuwa ni madini ambayo yanaathari kubwa katika mazingira na afya za binadamu.

"Tutambue kuwa kila Mradi unapotaka kuanzishwa katika Taifa letu unalazimika kufanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na mradi huu umefanyiwa toka 2012. Sisi kama Taasisi tumejiridhisha kuwa athari zake ni ndogo. Kimsingi mradi huu ulipewa kibali au cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira toka 2012 ambapo pia walikuwa hawajaanza kuchimba mpaka sasa hivyo pia tumekuja kujiridhisha kuhusu yaliyofanyika toka wapewe kibali hicho."Dkt.Gwamaka

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi NEMC Dkt. Catherine Masao amesema kuwa, kama mradi huu utazingatia taratibu walizoeleza na walizopewa na Baraza basi hautakuwa na athari ya kimazingira na kijamii.

"Mtazamo juu ya madini haya ya uraniam kwa wananchi bado ni mbaya hivyo kuna haja ya kutoa elimu kwa jamii ili kuelewa kwa undani wake. Mimi nikiwa kama mwakilishi wa kimazingira nimebaini athari zitokanazo na uraniam ni kutokana na kula na kuvuta kwa muda mrefu hivyo tutoe elimu kwa jamii watambue hili." Dkt. Catherine

Naye Fredrick Kibodya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited amesema kuwa, Mradi unafaida kubwa kwa jamii na kitaifa endapo utaanza utasaidia kutoa ajira kwa vijana kwani wanatarajia kuajiri watu wengi sana pamoja na hayo mradi utachangia mapato makubwa ya Taifa.

Ameendelea kusema kuwa wananchi wasiwe na wasiwasi na mradi kwa upande wa kimazingira na kiafya wamejipanga katika kudhibiti athari zote zitokanazo na uchimbaji wa uraniam, pia amesema kuwa kutokana na mradi huo kuwepo ndani ya Hifadhi watahakikisha miti na wanyama wanabaki salama.

Kwa upande wake Afisa muandamizi wa NEMC Muhandisi Dkt. Befrina Igulu amesema kuwa, NEMC ni Taasisi inayohusu mazingira itambulike kuwa uchimbaji wa madini ya uraniam unafanyika ndani ya Hifadhi hivyo unaweza kuathiri mazingira kwa namna moja ama nyingine, hivyo NEMC imekuja kuangalia namna gani utekelezaji wa mradi huo hauta athiri Mazingira.

Ameendelea kusema kuwa wananchi wasiwe na hofu juu ya utekelezwaji wa mradi huo, kwani serikali itasimamia na kuhakikisha maisha yao na viumbe hai vingine vinakuwa salama.
Share To:

Post A Comment: