Na Raphael Kilapilo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu (Mb), amesema Serikali ya Awamu ya Sita imetenga takribani shilingi bilioni 322 kwa ajili ya kujenga na kuboresha barabara za vijijini Nchi nzima, na kuwataka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha kuwa fedha hizo zinafungua barabara za maeneo yasiyofikika vijijini.

Waziri Ummy alisema hayo leo Julai 9, 2021 alipokagua ujenzi wa barabara mpya ya Kalalangabo – Lubabara iliyopo kata ya ziwani Halmashauri ya Wilaya Kigoma, katika mwendelezo wa ziara yake mkoani Kigoma kukagua miradi ya maendeleo.

Akikagua barabara hiyo, diwani wa Kata ya Ziwani Mhe. Zuberi Maftaha alimueleza waziri Ummy kuwa ujenzi wa barabara hiyo mpya ya kilomita mbili nukta tisa (2.9km) utagharimu shilingi milioni 24 na kuwapunguzia adha ya usafiri wananchi 2,455 wa Kijiji cha Kigalye wanaotumia usafiri wa maji kwa sasa.

“Sasa tulisema awamu ya sita inaenda kufungua barabara vijini, maana yake ndiyo hivi; katumia shilingi milioni 24 kwa hii barabara, lakini awamu ya sita imeweka bajeti ya maendeleo ya barabara za vijijini kwa jimbo la Kigoma peke yake, shilingi bilioni moja na milioni miatano (1.5 billion). Sasa angalieni  kama milioni 24 zimefungua barabara hii kwa wakazi wa kata ya ziwani, bilioni 1.5 zitafungua barabara ngapi za vijijini,“alisema Ummy.

Alieleza kuwa Billioni 322 zilizopangwa kufungua barabara za vijiji nchini kupitia TARURA zitachangwa na watanzania kupitia tozo mpya ya mitandao ya simu.

“Kwa hiyo mmeona, tunachangia kidogo lakini matokeo yake ni makubwa. Hivyo nikuahidi Mheshimiwa Mbunge barabara hii sasa tunaipiga changalawe ili ipitike wakati wote wa mwaka na wanachi hawa wasipate tena shida ya kupanda mitumbwi kufika Kigoma mjini. Hii ndiyo Serikali ya awamu ya Sita,” alisema Ummy.

Aidha Waziri Ummy alisema kuwa fedha hizi sasa zitaenda kupima utendaji kazi wa TARURA ambao walikuwa wakijitetea kuwa hawapati fedha ya kutosha hivyo kusababisha utendaji kazi hafifu.

“Tunataka sasa kuona kazi inafanyika kwa uaminifu, kwa ubunifu lakini kwa matokeo yanayoonekana. Mkahakikishe mnafungua barabara za maeneo yasiyofikika ili wananchi waione faida ya fedha hizi zilizotolewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan,”alisema Ummy.

Waziri Ummy aliwapongeza wabunge wa la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupigania kwa nguvu kubwa na kuhakikisha kuwa Serikali inajielekeza kutatua kero ya barabara za vijijini.
Share To:

Post A Comment: