Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa  Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi, akitoa maelezo kwa Maafisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA),  Shirika la Umoja wa Mataifa la  Maendeleo la Japani (KOICA) na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na usawa wa kijinsia na wanawake (UN Women) wakati wa ziara yao ya siku moja ya kukagua mradi walioufadhili uliopo katika Kata za Dung'unyi, Sepuka na Irisya wilayani Ikungi mkoani Singida ili kuona utekelezaji wake na matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa na Koica
Meneja Mwandamizi wa mradi kutoka Shirika la Farm Africa, Tumaini Elibariki (kushoto) akitoa maelezo  ya kilimo chenye tija cha zao la alizeti kwa maofisa hao.
Maofisa hao wakiwa kwenye kikao na wakulima (hawapo pichani) wa Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka. Kutoka Kulia ni Kaimu Mwakilishi Mkazi wa UN Women, Julia Broussaud, Kaimu Mkurugenzi Mkazi kutoka Koica, Jieun Mo na Mtaalamu wa Masuala ya Jinsia kutoka Shirika la UNFPA,  Maja Wanach. .
Mtaalamu wa Kitengo cha kuwawezesha Wanawake Kiuchumi kutoka UN Women, Lillian Madanga, akizungumzia mradi huo kwa ujumla wake.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi akizungumzia mradi huo jinsi utakavyo wanufaisha.
Mkuu wa Idara ya Uzalishaji wa TAHA, Gilliard Mollel, akitoa maelezo  ya kilimo cha mbogamboga na matunda kwa maofisa hao.
Ziara ya ukaguzi wa mradi huo ikiendelea.
Ukaguzi wa mradi huo ukiendelea.
Kaimu Mwakilishi Mkazi wa UN Women, Julia Broussaud, akiwaelekeza jambo maofisa wa shirika la TAHA. Kutoka kulia ni Mkuu wa Idara ya Uzalishaji wa TAHA, Gilliard Mollel, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi na Mratibu wa Mradi wa TAHA, Glory Prosper.
Wanawake wa Kipumbwiko wakiwa shambani wakati wa ukaguzi wa mradi huo.


Maofisa hao wakiwa kwenye kikao na wakulima (hawapo pichani) wa Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka.
Wakulima wa zao la Alizeti wa Kata ya Sepuka, Fatuma Said na Zainabu Hussein (kulia) wakionesha moja ya alizeti iliyostawi vizuri baada ya kuzingatia kilimo bora 
Meneja Mwandamizi wa mradi kutoka Shirika la Farm Africa, Tumaini Elibariki (kushoto) akitoa maelezo  ya kilimo chenye tija cha zao la alizeti kwa maofisa hao.
Wakulimawa Kata ya Irisya wakiimba nyimbo wakati wakiwakaribisha maofisa hao.
Shamba la mfano la mbogamboga la Kata ya Irisya.
Msaidizi wa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa  TAHA, Simon Mlay (kushoto) akitoa maelezo  ya kilimo cha mbogamboga na matunda kwa maofisa hao katika shamba la mfano la Kata ya Irisya.
Msimamizi wa Mashamba ya TAHA Mkoa wa Singida, Mohamed Bakari,  akitoa maelezo  ya kilimo cha mbogamboga na matunda kwa maofisa hao.
Wananchi wa Kata ya Irisya wakiwa shambani wakati wa ukaguzi huo.
Wananchi wa Kata ya Irisya wakiwa shambani wakati wa ukaguzi huo.. Kulia mwenye shati jeupe ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga na Diwani wa kata hiyo.

Mkulima wa Kijiji cha Kipumbwiko kutoka Kikundi cha Upendo, Rachel John, akizungumzia faida ya mradi huo.
Mkulima wa Kijiji cha Kipumbwiko kutoka Kikundi cha Jimudu, Elizabeth Myumbi, akiyashukutu mashirika hayo kwa kuwapelekea mradi huo.


Na Dotto Mwaibale, Singida


ZAIDI ya Wanawake  2300 wilayani Ikungi mkoani Singida wanatarajiwa kunufaika na mradi wa kilimo cha alizeti na mbogamboga kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA),  Shirika la Umoja wa Mataifa la  Maendeleo la Japani (KOICA) na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na usawa wa kijinsia na wanawake (UN Women)

Hayo yalibainika jana wakati wa ziara ya siku moja ya maofisa wa mashirika hayo ya kukagua mradi uliopo katika Kata ya Dung'unyi, Sepuka na Irisya wilayani hapa ili kuona utekelezaji wake na matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa na Koica ambapo wameridhishwa na utekelwezaji wa awamu ya kwanza wa mradi huo.

Mradi huo wa miaka mitatu ulioanza mwaka jana mkoani hapa unatekelezwa na mashirika hayo,  Serikali ya Tanzania,  Farm Africa na Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA katika mikoa ya Singida na Shinyanga.

Akizungumza katika ziara hiyo Mtaalamu wa Kitengo cha Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi kutoka UN Women, Lillian Madanga alisema wanafanya kazi hiyo kisera kwa kushirikiana na Serikali, Sekta binafsi na Halmashauri ambazo wana miradi hiyo yenye lengo la kuwainua wanawake kiuchumi kupitia kilimo cha mbogamboga matunda na alizeti.

Alisema katika kilimo cha mbogamboga na matunda wanafanya kazi na TAHA ambao wanauzoefu mkubwa na kilimo hicho hapa nchini kwa ufadhili wa Koica ambao wametoa fedha na kuwa kwa siku za mbeleni wananchi wa Ikungi watabadilika kimaendeleo kupitia kilimo hicho.

"Lengo letu kubwa la kuanzisha kilimo hiki na kuwapa teknolojia na kuwatafutia masoko ndani na nje ya nchi,"  alisema Madanga.

Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi akizungumza katika ziara hiyo aliishuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha hizo katika wilaya hiyo na kuwa watafanya kila liwezekanalo na kuona kilimo hicho kinanakuwa endelevu na kinawapeleka mbele.

Aidha Kijazi alisema kuwa mradi huo  utagharimu zaidi ya Sh.Bilioni 5.2 na kuwa umegawanyika katika aina kuu tatu, kilimo cha alizeti ambacho kinaongozwa na Farm Africa, Kilimo cha mbogamboga kinachoongozwa na TAHA na Mradi wa kuwawezesha wanawake kijinsia.

Alisema kwa mwaka huu wa mradi takribani dola 900,000 zimeruhusiwa na Koica na zinaendelea kufanya kazi katika maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.

Alisema mradi huo utakuwa kichocheo cha maendeleo katika halmashauri hiyo na kioo ambapo watatarajia kupata wawekezaji wengi baada ya kuona ardhi ya wilaya hiyo kuwa na rutuba ambayo kila aina ya mazao yanastawi.

Alisema jambo kubwa wanalolifanya hivi sasa ni upimaji wa ardhi katika vijiji vinne ambavyo wanavipima kupitia fedha za mradi huo ambavyo ni Kipumbwiko, Irisya, Munyu na Mnang'ana.

"Katika vijiji hivyo tunatenga maeneo mbalimbali  kwa ajili ya matumizi ya kilimo, makazi, misitu na ufugaji jambo litakalotusaidia kujua iwapo akitokea mwekezaji wa eneo husika kati ya haya yaliyotajwa tujue kwa kumpeleka," alisema Kijazi.

Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi alisema asasi hiyo yenye makao makuu yake jijini Arusha inafanya mradi huo Msalala mkoani Shinyanga na Ikungi mkoani Singida na imejikita zaidi kuwawezesha wadau katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mboga mboga, matunda, maua, viungo na mazao ya mizizi ambapo katika wilaya hiyo wameweza kuanzisha mashamba darasa . 

Alisema katika wilaya hiyo wameweza kuwapa wakulima teknolojia za kisasa za kilimo cha mbogamboga, matunda, maembe,vitunguu, pilipili kichaa, matumzi ya mbegu bora na kuwa wamepata soko nje ya nchi na mnunuzi wa mazao hayo zikiwemo pilipili atakazo zinunua kwa Sh.6000 kwa kilo.

Aliwataja wadau wanao wawezesha katika mnyororo huo wa thamani kuwa ni wasambazaji wa pembejeo, wakulima, wasindikaji, wafanyabiashara, wasafirishaji na makampuni yanayofanya usafirishaji nje ya nchi na wanawawezesha kwa vitendo.

"  Katika uwezeshaji wetu kazi kubwa tunazozifanya ni kuwaunganisha wakulima na masoko, kuwawezesha wakulima katika suala zima la kilimo na kuwaonesha teknolojia mbalimbali ambazo wanaweza kuzitumia kulingana na uwezo na mazingira waliopo." alisema Mkindi.

Alitaja kazi ya nyingine kuwa ni kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara na kuwa wanafanya kazi hiyo kwa kushirikiana kwa karibu na serikali kuu kwa maana ya kushawishi na kutetea sera zile ambazo zinamuumiza mzalishaji, mfanyabiasha na mdau yeyote katika mnyororo wa thamani.

Aidha Mkindi alitaja kazi nyingine kuwa ni kuwaunganisha wadau katika mnyororo wa thamani na vyombo vya fedha baada ya kuwafundisha elimu ya fedha.

Share To:

Post A Comment: