Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amesema ataweka utaratibu mahususi kwa ajili ya kupitia maagizo, ushauri na maoni ya Mkaguzi wa ndani wa Halmashauri za Mkoa huo kujiridhisha makosa yanayojitokeza na kusababisha hoja za kiukaguzi na kujua kiini cha mapungufu hayo.

Martine Shigela amesema hayo Juni 10 mwaka huu wakati wa kikao cha Baraza Maalum la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi kwa ajili ya kupitia hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali – CAG ikiwa ni mwendelezo wa kushiriki mabaraza hayo kwa mujibu wa maagizo ya Serikali.

Shigela amesema, Mkaguzi wa ndani ndio jicho la Mkurugenzi na Halmashauri nzima kwa jumla, ambaye anatakiwa ashauri, atoe maoni yake na kuonesha mapema mapungufu yanayotaka kujitokeza au yaliyoanza kujitokeza ndani ya Halmashauri ili kuepusha hasara kwa serikali inayoweza kujitokeza.

“Internal Auditor wetu ndio jicho la Halmashauri, ndio pua ya Mkurugenzi, ndio masikio ya Mwenyekiti na ndio miguu ya Halmashauri yetu” amesema Martine Shigela.
Kwa sababu hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema yuko katika mikakati ya kuweka utaratibu wa kupitia maoni na ushauri wa Mkaguzi wa ndani wa kila Halmashauri, lengo ni kutaka kujua kama matatizo yanayojitokeza katika Halmashauri yanatokana na Mkaguzi wa ndani ama uongozi wa Halmashauri.

“na mimi nataka nisema hapa, nitaweka utaratibu, wa  kila miezi mitatu kufahamu kuwa Internal Auditor amesema nini, na halmashauri imechukua hatua gani, ili tujue tatizo liko kwa Internal Auditor au liko kwenye Menejimeti” amesisitiza Shigela.
Katika hatua nyingine Martine Shigela ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mkoani humo kutoruhusu matumizi ya fedha za Serikali yasiyo na nyaraka za fedha zilizotumika.

“Naomba sana wahe. Madiwani na Mkurugenzi akiwepo hapa, sitaki tena jambo hili lijirudie  mwaka ujao wa fedha – Shigela.

Amesema,  utaratibu wa matumizi ya fedha yasiyo na nyaraka unaweza kupelekea kwa baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waaminifu kuweza kutumia mwanya huo kutumia fedha za Serikali kwa maslahi yao binafsi  na kuathiri utekelezaji wa mipango ya Serikali ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja ameahidi kusimamia maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kuyatekeleza huku akisisitiza watumishi wa Umma ndani ya Mkoa huo kuwa na ushirikiano na kuwajibika katika majukumu yao.

Mkuu wa Wilaya ya Malinyi  Mathayo Maselle yeye  ameeleza namna Uongozi wa Wilaya hiyo unavopambana na kutatua changamoto za wananchi ikiwemo upatikanaji wa nishati ya umeme, ubovu wa barabara pamoja na wananchi kuwa mbali na vituo vya kutolea huduma za Afya.

Share To:

Post A Comment: