Na Loema Joseph, (TPC).

 

Waziri wa Wawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe.Dkt. Faustine Ndugulile amelitaka Shirika la Posta Tanzania kukusanya madeni kutoka kwa watu wote wanaotumia milki za Shirika (Wapangaji) ikiwemo majengo na viwanja kulipa kodi zao ndani ya miezi mitatu na kinyume na hapo hatua za kuondoa watu hao zichukuliwe.

 

“Watu wote wanaokaa kwenye milki za shirika wanapaswa kulipa kodi na watu ambao hawajalipa waondolewe,nakupa miezi mitatu,kuhakikisha wenye madeni wawe wamelipa kikamilifu kwa sababu hatuwezi kuona watu wanatumia rasilimali za Shirika na hawalipi” Alisema Dkt. Ndugulile.

 

Ameyasema hayo leo tarehe 1 Juni, 2021 wakati akifanya kikao kazi na menejimenti ya Shirika la Posta nchini, mara baada ya kufanya ziara yake ya kikazi kutembelea ofisi na milki na rasilimali zinazomilikiwa na Shirika la Posta, jijini Dar es salaam pamoja na kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa kwa Menejimenti hiyo alipolitembelea Shirika mwezi Januari,2021.

 

Aidha,Mhe. Dkt.Ndugulile amelitaka Shirika kubadilika ili kuendana na kasi ya sasa ya dunia,pia kuendana na matakwa na mahitaji ya wananchi kwa kujikita zaidi kwenye mabadiliko ya utendaji mikakati,mitizamo ndani ya taasisi pamoja na bidhaa na huduma zitolewazo  na Shirika kwa wananchi.

 

Sambamba na hilo amewataka wafanyakazi wa Shirika la Posta kutimiza majukumu yao kwa wakati na hasa kuhakikisha ufanisi katika maeneo wanayosimamia kwa lengo la kuleta matokeo chanya kwa taasisi na taifa kwa ujumla. Alisisitiza ushirikiano “Teamwork”, katika maeneo ya kazi kwa kuwa wafanyakazi wote wanawajibika kwa umma na sio mtu binafsi hiyo italeta ufanisi.

 

“Sipendi kutuma mtu kazi nataka kila mtu ujitume kwenye majukumu yake katika eneo analolisimamia ahakikishe anawajibika katika kuleta matokeo chanya ndani ya taasisi yetu jengeni “Teamwork” katika kuyatimiza haya”. Alisema.

 

Kwa upande wake kaimu Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo amemshukuru Mhe.Dkt Faustine Ndugulile kwa kutenga muda wake na kuja kuwatembelea, Ameshukuru na kusema ameyapokea maagizo yaliyotolewa na Mhe.Waziri na kwa kushirikiana na menejimenti ya Shirika ameahidi kuyafanyia kazi usiku na mchana katika kuhakikisha malengo ya Shirika na Serikali yanafiikiwa.

 

“Mhe.Waziri kwanza nikushukuru kwa kututembelea na kwa maelekezo uliyoyatoa,tumeyapokea na tunakuahidi kwamba tunaenda kuyafanyia kazi kama ulivyoelekeza.”. Alisema  Bw.Mbodo.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: