.Na. Catherine Sungura,WAMJW,Kagera


Viongozi wa ngazi ya Mkoa, Wilaya na Halmashauri  wametakiwa kuwahamasisha wananchi kwenye maeneo yao husuan kwenye kupambana na kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwani changamoto zozote za afya zinaathiri moja kwa moja uchumi.


Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia     Jenerali Marco Gaguti wakati wa kikao kazi cha uraghibishaji na uhamasishaji wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD) kwa viongozi wa Mkoa,Wilaya na halmashauri zote za Kagera kilichoandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele.


“Changamoto zozote za afya zina athiri moja kwa moja uchumi, kama sisi viongozi tusipokuwa na afya hatutoweza  kutoa huduma  kwa usahihi kwa watu tuliopewa dhamana ya kuwasimamia maendeleo yao”.


Aliongeza kuwa kama jamii inakwazwa kwa njia moja au nyingine inaathiri muda wa wananchi na utoaji wa nguvu zao kwenye tija ya kazi wanazozifanya kwani magonjwa hayo kwa watu wazima hawayaoni kama ni ajenda muhimu bali wamekuwa wakipigania kwa watoto chini ya miaka mitano.


“Sisi watu wazima hatuoni kama  ni ajenda  muhimu kupambana na magonjwa haya na tumekuwa tunapigania kwa watoto chini ya miaka mitano,niendelee kutoa msisitizo kwa wana Kagera kuona umuhimu wa kuunga mkono jitihatazda za Serikali kwa watanzania kuwa wenye afya njema kwani wanatoa mchango mkubwa kwenye kazi zetu zinafikiwa”.


Hata hiyo Mkuu huyo wa mkoa aliwataka viongozi wa mkoa huo kuendelea kushirikiana na wadau wote na endapo wadau hao wataondoka basi mkoa utasimama wenyewe na hivyo kuwataka kutenga bajeti za fedha za ndani za kupambana na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele na yale mengine ambayo yanaathiri shughuli za utendaji wa kila siku.


Aidha, Mhe. Gaguti amewataka viongozi hao kuimarisha elimu ya afya pamoja na usimamizi wa kusimamia afya kwa kufanya ukaguzi kwenye maeneo yote ya huduma za kijamii pamoja na makazi ya wananchi kwa kuzingatia usafi wa mazingira pamoja na unawaji wa mikono .


Amesema udhibiti wa magonjwa kwa  wananchi itakuwa na manufaa makubwa kwa kuishi maisha marefu,na kuepuka matumizi ya dawa ya mara kwa mara na pia kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi kwa kujikinga na maradhi hayo.


Hata hivyo ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuandaa kikao kazi hicho kwani kama mkoa wamekuwa wakitekeleza jitihada za kupambana na kudhibiti magonjwa mbalimbali hivyo kwa magonjwa hayo ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele ni muhimu sana katika kupigania afya za watanzania.


Naye Mwakilishi wa Mratibu wa Taifa wa Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Wizara ya Afya Bw.Oscar Kaitaba amesema kama mpango wana lengo la kuwawezesha wananchi kuwa na afya bora na kwa mkoa wa kagera wanatoa kinga tiba ya  kichocho na minyoo ya tumbo kwa watoto wenye umri wa kwenda shule (walioandikishwa na wasioandikishwa) kuanzia miaka 5 hadi 14.


Wakati huo huo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dkt. Issessanda Kaniki amesema zoezi la ugawaji kinga tiba linahitajika sana kwenye mkoa huo katika halmashauri zote nane na hivyo mkoa umejipanga kutekeleza zoezi hilo kwa  uhamasishaji kuanzia ngazi ya viongozi na jamii .


Dkt. kaniki amesema kwa upande wa usafi wa mazingira amesisitiza wananchi kuzingatia usafi wa mazingira kwenye maeneo yao ya makazi pamoja na vituo vyote vya kutolea huduma za kijamii ili kuepuka na magonjwa yanayosababishwa na uchafu na kuwataka wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya vyoo, kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni na kuzingatia lishe bora ili kuepuka na magonjwa.


Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi kipaumbele inatarajia kuanza ugawaji wa kinga tiba kwa Mkoa wa Kagera kuanzia tarehe 24 hadi 28 Mei mwaka huu.

-MWISHO-

Share To:

msumbanews

Post A Comment: