Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akiuliza jambo baada ya kupatiwa ufafanuzi juu ya uchakataji wa minofu ya samaki kutoka kwa mmoja wa viongozi wa kiwanda cha Victoria Perch Limited kilichopo jijini Mwanza, mara baada ya kutembelea kiwanda hicho kufahamu upatikanaji wa malighafi, uzalishaji na masoko. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akiangalia makasha mbalimbali yenye minofu ya samaki yakiwa tayari kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi, mara baada ya kutembelea kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki cha Tanzania Fish Processor kilichopo jijini Mwanza. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza na viongozi wa kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki cha Tanzania Fish Processor kilichopo jijini Mwanza pamoja na maafisa kutoka wizarani mara baada ya kutembelea kiwanda hicho ili kufahamu upatikanaji wa malighafi kiwandani hapo. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Na. Edward Kondela

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amewaelekeza viongozi wa viwanda vya kuchakata samaki Mkoani Mwanza kukaa na maafisa kutoka katika wizara hiyo kutafuta suluhu ya ukosefu wa malighafi ya kutosha katika viwanda vyao ili viweze kufanya kazi kwa kadri ambavyo vinatarajiwa.

Naibu Waziri Ulega amesema hayo jana (23.05.2021) wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo kwa kutembelea viwanda vya kuchakata minofu ya samaki vya Tanzania Fish Processor na Victoria Perch Limited baada ya kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya viongozi wa viwanda juu ya ukosefu wa malighafi ya samaki aina ya sangara.

Akiwa katika nyakati tofauti kwenye viwanda hivyo naibu waziri huyo ameambiwa na viongozi wa viwanda kuwa upatikanaji wa samaki umeendelea kuathiri shughuli za viwandani na kuongeza gharama za uzalishaji na kuiomba serikali kuangalia namna ya kuwasaidia katika kutafuta suluhu ya upatikanaji wa malighafi hizo.

Akitoa maelezo ya jumla mara baada ya kuzungumza na viongozi wa viwanda Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema ukosefu wa malighafi unadaiwa kupungua viwandani kutokana na vitendo vya uvuvi haramu, biashara ya mabondo na bei ndogo ya samaki wanaonunuliwa katika viwanda hivyo na kuelekeza viongozi wa viwanda na maafisa kutoka wizarani kukaa pamoja na kubaini kiini hasa cha tatizo hilo ili kutafuta suluhu.

“Sisi tunafurahi tukisikia wananchi wanapata, wakati huo tunataka viwanda vipate malighafi yote mawili tunayataka lazima tuwe na nyongeza ya maarifa ili tupate suluhu ya jambo hili tutoke kwa mafanikio wote wafurahi.” Amesema Mhe. Ulega

Ameongeza kuwa uwepo wa viwanda vya kuchakata samaki unalinufaisha taifa kwa kuwa serikali inapata mrabaha wa mazao yanayoenda nje ya nchi ambapo fedha hizo zinatumika katika shughuli mbalimbali zikiwemo za kijamii.

Kuhusu kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu amesema wizara imejipanga vyema na kuwataka watu wote wanaojishughulisha na vitendo hivyo kuacha mara moja na kwamba serikali itaongeza juhudi za kupambana na uvuvi haramu na kutaka ushirikiano kutoka kwa kila mdau.

Amefafanua kuwa wizara imepanga utaratibu wa kutambua hatua mbalimbali za upatikanaji wa nyavu za uvuvi tangu kutengenezwa kwake hadi kusambazwa na kumfikia mvuvi ili kudhibiti usambaaji wa nyavu zisizohitajika kisheria hapa nchini.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Mwanza kwa kuonana na baadhi ya wavuvi katika Wilaya ya Sengerema na kuzungumza nao juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili pamoja na kutembelea viwanda vya kuchakata minofu ya samaki Jijini Mwanza ili kujionea upatikanaji wa malighafi ya samaki aina ya sangara.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: