Mkutano mkuu Umoja wa mafundi cherehani wa mkoa wa Dodoma (UMACHEDO) umefanyika jana katika hoteli ya Dodoma kwa mafanikio makubwa huku ukihudhuriwa  na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dr.Hashil Abdallah (kwa niaba ya  Mh. Waziri Prof. Kitila Mkumbo),Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh. Anthony Mtaka na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde.


Akizungumza kwa niaba ya Wizara  Viwanda na Biashara,Naibu Katibu Mkuu Dr. Hashil Abdallah amewapongeza mafundi cherehani wa Dodoma kwa kuja na wazo la kuunda umoja wao na kutumia fursa hiyo kuwaahidi mafundi hao kupata mikopo kupitia mfuko wa wajasiriamali (NEDF) uwezeshwaji wa vyerehani kwa mikopo nafuu na semina mbalimbali za mafunzo kupitia SIDO.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh.Anthony Mtaka amewapongeza UMACHEDO kwa kuungana pamoja na kuwataka kuchangamkia fursa zilizopo Dodoma badala ya kuwa waangaliaji wa fursa zilizopo Dodoma na kuwahakikishia ushirikiano kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuwawekea mazingira rafiki katika utoaji wa huduma zao katika shughuli mbalimbali za kiserikali zikiwemo mbio za Mwenge.


Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde ambaye pia ni Mlezi wa UMACHEDO ameahidi kuwaunganisha mafundi hao na Taasisi za NSSF,SIDO na NHIF kwa lengo la kuwanufaisha zaidi wananchama na kuahidi kusimamia kwa karibu upatikanaji wa mashine za kisasa za kushonea  kupitia mkopo utokanao na Mfuko wa Taifa wa Wajasiriamali (NEDF) na Benki ya Azania.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: