Diwani wa Kata ya Mang'onyi, Wilaya ya Ikungi,  Innocent Makomelo akitoa shukurani kwa  Meneja wa Kampuni ya Uchimbaji  Dhahabu ya Shanta Mradi wa Mkoa wa Singida, Jiten Divecha (kulia) na kwa viongozi wa wilaya hiyo kwa msaada wa madawati 183 yaliyotolewa na kampuni hiyo kwa Shule ya Sekondari ya Mang'onyi Shanta katika hafla iliyofanyika jana.


Diwani wa Kata ya Mang'onyi, Wilaya ya Ikungi mkoani hapa Innocent Makomelo akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwau  jana wakati akikabidhi madawati 50  ikiwa ni mwanzo wa jitihada zake katika kukabiliana na kero ya watoto kukaa chini.


Diwani wa Kata ya Mang'onyi, Wilaya ya Ikungi mkoani hapa Innocent Makomelo akisisitiza jambo wakati akizungumza  hao.
 


Na Waandishi Wetu, Singida.


KASI ya utendaji ndani ya mfumo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake vinazidi kudhihirika kwa vitendo kupitia wateule na watendaji wake mbalimbali, ambapo mapema jana Diwani wa Kata ya Mang'onyi, Wilaya ya Ikungi mkoani hapa Innocent Makomelo alikabidhi madawati 50 kwa Shule ya Sekondari Mwau ndani ya eneo hilo, ikiwa ni mwanzo wa jitihada zake katika kukabiliana na kero ya watoto kukaa chini.

Sambamba na tukio hilo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo naye alipokea jumla ya madawati 183 na taarifa ya umaliziaji wa ukarabati wa vyumba 5 vya madarasa vyenye hadhi ya aina yake, kwenye shule ya Sekondari Mang'onyi Shanta iliyopo ndani ya Kata ya Diwani huyo.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati akishiriki matukio hayo, Makomelo  alipongeza kasi ya serikali na wadau wa maendeleo kwa namna wanavyoitazama Mang'onyi kwa jicho la kipekee, huku akiahidi kumaliza kabisa kero sugu kwenye maeneo hayo, ili kuchagiza kasi ya maendeleo.

Alisema kutokana na dhamira njema ya serikali kwenye eneo la utoaji huduma ya elimu bure kuanzia darasa la Kwanza mpaka Sekondari imepelekea wazazi wengi kuhamasika kuwaleta watoto shuleni, hali iliyosababisha msongamano na uhaba wa viti na meza uliopo.

"Hata hivyo juhudi nyingine za kumaliza changamoto hii zinaendelea kwa kasi kubwa ili kuweka mazingira mazuri ya watoto kujisomea ili waweze  kupandisha zaidi ufaulu wao. Tumeanza na madawati haya 50 na mengine yatafuata," alisema Makomelo.

Aidha, alishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kupeleka shilingi milioni 100 kwenye shule hiyo kupitia EPFR (Education Performance for Results) kutokana na kuwa miongoni mwa shule zilizofanya vizuri kwenye ufaulu.

"Msome kwa bidii na sisi viongozi tutahakikisha tunatimiza nahitaji yenu. Ufaulu wenu ndio sababu iliyopelekea serikali kuwaletea fedha hizo ambazo zimewasaidia kujenga madarasa 2 na ofisi ya mwalimu. Mkifanya vizuri zaidi ndivyo tutakavyoendelea kupata fedha nyingi zaidi," alisema Diwani Makomelo wakati akikabidhi madawati hayo.

Kuhusu changamoto ya maji na miundombinu yake ya usambazaji kwa baadhi ya maeneo, alisema kwa sasa kero hiyo inaendelea kushughulikiwa na muda mfupi ujao suala hilo litapatiwa ufumbuzi.

Aidha, kwa namna ya pekee, Diwani huyo alipongeza ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka kwa Mbunge wa Jimbo hilo, Miraji Mtaturu, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kwa namna wanavyojitoa kuhakikisha ustawi wa maendeleo kwa wanamang'onyi unafikiwa.

"Mambo mengi makubwa yanakuja chini ya serikali hii ya Mama Samia Suluhu Hassan. Lakini kubwa zaidi ni mchakato unaoendelea vizuri wa kuratibu ajira za kutosha kwa wakazi wa Mang'onyi na maeneo mengine yanayozunguka mgodi huo," alisema Makomelo.

Share To:

Post A Comment: