TIMU ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefika katika Kata ya Kibwigwa Jimbo la Buhigwe ambapo wamemuombea kura mgombea Ubunge wa CCM.


Wabunge hao ni Mariam Ditopile wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma na Cecil Mwambe wa Jimbo la Ndanda mkoani Mtwara ambapo wamewaomba wananchi wa Kata ya Kibwigwa kumpigia kura mgombea huyo wa CCM, Javejuru Felix katika uchaguzi huo utakaofanyika Jumapili ya Mei 16 mwaka huu.


Akizungumza katika mkutano huo, Mariam Ditopile amewataka wananchi hao kumchagua mbunge wa CCM ili aweze kushirikiana na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango ambaye awali alikua mbunge wao pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza miradi iliyokua  imeanza kutekelezwa.


" Kibwigwa na Buhigwe kwa ujumla imeshapata neema ya kuwa na Makamu wa Rais sasa ili kasi ya kimaendeleo izidi kusonga mbele ni lazima tumchague Mbunge wa CCM ambaye ataenda kuzungumza lugha moja na Rais Samia na Dk Mpango.


Huyu Mgombea wa ACT hawezi kumfikia Dk Mpango wala Rais Samia kwenda kuomba fedha za miradi, Zito Kabwe anawadanganya tu, hata mke wa kuoa alikosa ACT akaamua kuja kuoa CCM kama Chama chake kina maana angeoa huko lakini alikimbilia kuoa CCM, " Amesema Ditopile.


Kwa upande wake Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwamba amesema wapinzani wa Nchi hii wamejaa ulaghai na wanachokitafuta ni kwa ajili ya matumbo yao na siyo maendeleo ya wananchi na ndio maana wamekua wakipinga hata miradi ya maendeleo inayofanywa na Serikali.


" Nilikua upinzani tena Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, kilichoniondoa upinzani wakati Serikali ikitekeleza miradi ya maendeleo sisi kazi yetu ilikua kugombana kila siku.


Buhigwe mmepata bahati ya kuwa na Makamu wa Rais Dk Mpango sasa ili mumpe heshima Rais Samia ni kumletea Mbunge wa CCM ambaye atakua anawasemea kwake kuhusu miundombinu ya barabara, vituo afya na mtu huyo ni Kavejuru pekee, " Amesema Mwambe.


Share To:

msumbanews

Post A Comment: