Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Ndg. Daniel Chongolo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China Nchini Tanzania Bi. Wang Ke.


Mazungumzo hayo yamefanyika leo tarehe 31 Mei, 2021 katika ofisi za Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma, ambapo Balozi huyo anayemaliza muda wake nchini Tanzania ametumia fursa hiyo kuwaaga wanaCCM na watanzania kwa ujumla, ambapo ameeleza kuwa, China na Mataifa mengine yanafurahishwa sana na mwenendo mzuri wa uongozi wa awamu ya sita chini ya Rais na Mwenyekiti wa CCM Mhe. Samia Suluhu Hassan na wanatarajia Tanzania kuendelea kupiga hatua zaidi za maendeleo.


"Tunafuraha kuona kwamba, uongozi mpya ndani ya Chama na Serikali chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu  Hassan unaendelea vema na uongozi umendelea kuwa imara na wenye tija kwa wananchi wake.  Pia uongozi unaendelea kupata ushirikiano mkubwa sio tu ndani ya nchi bali na nje ya Tanzania. Hivyo tunaamini Tanzania itaendelea kupiga hatua zaidi za kimaendeleo." Balozi Wang Ke.


Balozi huyo, kwa niaba ya serikali na watu wa China amemuhakikishia Katibu Mkuu kuwa, wataendelea kutoa ushirikiano wote kwa upande wa Serikali na Chama  hasa kutokana na historia nzuri iliyopo kati ya CCM na Chama Cha Kikomunisti cha China CPC.


Aidha, ametumia fursa hiyo kuipongeza CCM kwa kuvuka salama, kwa amani na utulivu mkubwa katika kipindi kigumu cha kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Dkt. John Pombe Magufuli, na kufanikiwa kumpata mwenyekiti mpya na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.


Wakati huo huo kwa upande wa Katibu Mkuu kwa niaba ya CCM ameitumia fursa hiyo kumuomba Balozi Wang Ke, kuendelea kuwa balozi mzuri wa Tanzania nchini China kwa kuwa yeye amepata bahati ya kuishi hapa, na kujionea mwenyewe utulivu na amani iliyopo nchini.


Pia, Katibu Mkuu amemuhakikishi Balozi kuwa, ushirikiano kati ya Tanzania na China, na kati ya CCM na CPC sio wa kutiliwa mashaka, ni uhusiano wa kindugu na umejengwa katika misingi ya kihistoria na kamwe hauwezi kutetereshwa.


Kikao hiko kimehudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM wakiwemo Naibu Katibu Mkuu Bara Bi. Christina Mndeme, Katibu wa NEC, Oganaizesheni Bi. Moudlin Cyrus Castico, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndg. Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Dkt. Hawasi Haule na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania UWT Mwl. Queen Mlozi.


Imetolewa na;


Said Said Nguya

Afisa Habari

Ofisi ya Katibu Mkuu

CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)

Share To:

msumbanews

Post A Comment: