Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu,akizungumza na Mzazi ambaye alikuwa amempeleka mtoto katika hospitali ya Uhuru iliyopo Wilaya ya Chamwino Dodoma wakati wa ziara ya kukagua Maendeleo ya hospitali hiyo leo April 14,2021. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu,akisikiliza taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ambaye alikuwa msimamizi wa ujenzi Athumani Masasi (katikati) ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge wakati wa ziara ya kukagua Maendeleo ya hospitali ya Uhuru iliyopo Chamwino Mkoani Dodoma leo April 14,2021. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu,akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ambaye alikuwa msimamizi wa ujenzi Athumani Masasi (katikati) ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge wakati wa ziara ya kukagua Maendeleo ya hospitali ya Uhuru iliyopo Chamwino Mkoani Dodoma leo April 14,2021. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu,akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua na kujionea  Maendeleo ya hospitali ya Uhuru iliyopo Chamwino Mkoani Dodoma leo April 14,2021. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu,akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Uhuru iliyopo Chamwino Mkoani Dodoma mara baada ya kukagua na kujionea Maendeleo ya Hospitali hiyo leo April 14,2021. 
Muonekano wa jengo la Hospitali ya Uhuru iliyopo Chamwino Mkoani Dodoma.

Mkuu wa Shule ya Watu Wenye Mahitaji Maalumu ya Buigiri inayomilikiwa na Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika Mwl.Samwel Jonathani akisoma risala kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe.Ummy Mwalimu (hayupo pichani) ambaye alifanya ziara shuleni hapo leo April 14,2021. 

 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu,akifanya ziara ya kukagua Miundombinu ya  Shule ya Watu Wenye Mahitaji Maalumu ya Buigiri inayomilikiwa na Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika  leo April 14,2021. 
……………………………………………………………………………………………………

Na.Alex Sonna,Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu amefanya ziara katika hospitali ya Uhuru iliyopo Wilaya ya Chamwino kukagua Maendeleo yake na kuagiza kuanza ujenzi wa majengo ya  awamu ya pili ili kupanua zaidi wigo wa upatikanaji wa huduma za afya.

Akizungumza mara baada ya kumaliza kukagua maendeleo katika hospital hiyo Waziri Ummy amesema mara baada ya baadhi ya huduma kuanza kutolewa sasa waanze mchakato wa ujenzi wa majengo ya awamu ya pili yatakayojumuisha na wodi za kulaza wagonjwa.

“Sasa hapa tumeona kazi kubwa imefanyika zimebaki kazi ndogo ndogo ili ujenzi wa awamu ya kwanza ukamilike, naona na huduma zinatolewa, sasa tuanze mchakato wa ujenzi wa awamu ya pili tujenge mawodi hapa ni barabarani lazima tupanue zaidi huduma” amesema Waziri Ummy.

Amesema hospital hiyo ni kubwa sana na inahudumia mpaka Mikoa na Wilaya za karibu hivyo ni muhimu ujenzi wa awamu ya pili ukamilike kwa wakati kuwapunguzia wananchi kupata huduma mbali ambapo kwa sasa baadhi ya huduma wanafuata hospitali ya rufaa Dodoma na Benjamini Mkapa.

Amesema Serikali ya sasa itayaendeleza mambo yote yaliyoanzishwa na hayati Dkt Magufuli ambapo sasa watatoa kiasi cha shilingi bilioni 1.7 zinazohitajika ili kukamilisha kazi ndogo ndogo zilizobaki kukamilisha awamu ya kwanza ya and ujenzi.

Amewakata watumishi katika hospitali hiyo kufanya kazi kwa weredi na kufuata maadili ya kazi yao wanapotoa huduma kwa wananchi na kutoa kauli nzuri kwa wagonjwa wanapowahudumia.

Pia ametaka watumishi katika hospitali hiyo na watumishi wengine kuwahamasisha wananchi kujiunga katika mfuko wa bima ya afya kuwapunguzia gharama za matibabu wanapougua.

“Tuwahamasishe wananchi wajiunge na mfuko wa bima ya afya, ukiangalia kuna wagonjwa kujiandikisha tu anatoa elfu kumi na tano (15,000) wakati angekuwa na bima hata ile ya elfu thelathini(30,000) asingelipa hiyo elf kumi na tano” amesema.

Aidha amewatoa hofu watumishi wanaofanyakazi za kujitolea katika hospitali kuwa serikali itawapa kipaumbele katika katika ajira zitakazotolewa huku akitaka kuwe na kanzi data ya watumishi wanaojitolea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

“Naagiza Waganga wakuu wa Wilaya mkasimamie hilo na kwenye data base (kanzi data) watumishi hao waainishwe kaanza kujitolea lini, isije kuwa kesho wakafurika watu wa kujitolea baada ya kusikia watapewa kipaumbele kwenye ajira” amesema.

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ambaye alikuwa msimamizi wa ujenzi Athumani Masasi amesema ujenzi ulianza rasmi Novemba 26, 2019, kwa kutumia force akaunti kwa kutumia mkandarasi SUMA JKT na mpaka sasa Ujenzi wake umefikia asilimia 98.2.

Amesema  Hospitali hiyo imeanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje tangu Desemba 21, 2020 na inawatumishi 52 kati ya watumishi 117 wanaohitajika, na mpaka sasa imehudumia wagonjwa 3,154, na tayari imekusanya zaidi ya milioni 33.

Ujenzi wa hospital ya Uhuru ni matokeo ya matokeo ya kuahilishwa kwa sherehe za uhuru mwaka 2018 na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Dkt Magufuli na kuagiza fedha hizo ziende katika ujenzi wa Hospitali hiyo.

Waziri Ummy pia amefanya ziara katika shule ya watu wenye mahitaji maalumu ya Buigiri inayomilikiwa na Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika kwa kushirikiana na Serikali na ameahidi ushirikiano huo utaendelea kudumu.

Pia amebainisha kuwa watatoa kila ushirikiano kwani ni dhamira ya Serikali kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalumu wanapata huduma ya elimu katika ngazi mbalimbali.

Nae Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Samwel Jonathani amesema shule hiyo inawanafunzi 118 wenye ulemavu mbalimbali na kubainisha kuwa wanafunzi hao wamekuwa na ufaulu wa asilimia 98 hadi 100 kwa miaka kumi mfululizo.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: