Askofu wa Jimbo Katoliki la Kondoa Mhashamu Bernadin Mfumbusa, akiongoza adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi wa sherehe za Jubilei ya miaka 50 ya Jimbo Katoliki Singida jana.

Maaskofu, Mapadre, Watawa na Waamini wengine wakishiriki kwa furaha moja ya tukio la Jubilei hiyo la kurusha ‘Njiwa wa  Amani’ hewani kama ishara ya jukumu la kitume katika mwendelezo wa kazi aliyowaachia Yesu Kristu ya kusambaza Habari Njema, Umoja, Amani na Mapendo kwa mataifa.

Askofu wa Jimbo Katoliki Singida Edward Mapunda akimkabidhi mmoja wa mapadre wa Jimbo hilo Msalaba kama ishara ya bendera ya ushindi ili akatangaze ushindi huo kwa Kristu aliyekubali kuteseka, kufa na baadaye kufufuka. 

Mapadre na Waamini wa Jimbo Katoliki Singida wakishiriki Ibada hiyo.

Maaskofu Bernadin Mfumbusa (kushoto) na Edward Mapunda (kulia) wakiwa wameshika Mshumaa wa Jubilei ya dhahabu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jimbo Katoliki Singida.

Watawa wa kike kutoka mashirika mbalimbali yanayofanya utume jimboni humo wakishiriki adhimisho la Ibada hiyo.

Ibada ikiendelea.

Kiongozi wa Kwaya ya Shirikisho Jimbo Katoliki Singida Peter Jihango akiongoza kwaya hiyo katika adhimisho hilo.


Katibu wa Liturjia Jimbo Katoliki la Singida, Padre Paterni Mangi, akishiriki kuwasha mshumaa wa Jubilei hiyo.

Maaskofu na Mapadre wakiwa kwenye picha ya pamoja muda mfupi baada ya adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi wa sherehe za Jubilei ya miaka 50 ya Jimbo Katoliki Singida.



Dotto Mwaibale na Godwin Myovela, Singida


JIMBO Katoliki Singida limeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi kuelekea kilele cha Jubilei yake ya dhahabu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Jimbo hilo liliundwa na Baba Mtakatifu Paulo wa VI kutokana na majimbo ya Mbulu, Dodoma na Tabora mnamo Machi 25, 1972 (Sikukuu ya Kupashwa Habari Bikira Maria), ambapo kilele cha maadhimisho hayo ni ifikapo Agosti 21, 2022.

Akiongoza adhimisho la Ibada hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa, Mhashamu Bernadin Mfumbusa pamoja na mambo mengine, alisema Jubilee ni kipindi cha sala na shukrani kwa Mungu kwa wema na ukarimu, kujitathmini, kuanza upya, kuwa na matumaini na kusamehe.

Aidha, alisema Umoja na Mapendo iwe ni tunu na dira muhimu katika Jubilei hiyo katika muktadha chanya wa kutangaza na kumwilisha huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha.

"Msiogope kila kitu kinawezekana. Ni kipindi kizuri cha kujitathmini tunatoka wapi na tunaelekea wapi...Mungu akiwepo chochote kinawezekana," alisema Askofu Mfumbusa.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Jimbo, Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, Mhashamu Edward Mapunda kupitia Jubilei hiyo yenye Kauli Mbiu isemayo  'Jubilei Singida-Umoja na Mapendo,' aliwashukuru wamisionari wote waliojisadaka na kushuhudia habari njema bila ya kujibakiza katika kipindi chote.

Hata hivyo, Askofu Mapunda alihimiza waamini kushiriki kikamilifu mpango dira wa matukio yaliyoandaliwa kuelekea kilele cha Jubilei hiyo ili kujiweka zaidi mikononi mwa Mungu na kumshukuru kwa zawadi ya Jimbo na Imani.

Baadhi ya matukio yaliyopo ndani ya mpango huo ni kusali, novena, mafungo, semina, hija, matembezi ya Msalaba, matendo ya ukarimu, kuanzisha na kuimarisha vyama vya kitume, kuhamasisha miito ya utawa na upadre, katekesi endelevu na kutolewa msamaha kwa masuala mbalimbali ya kiroho-ikiwemo ubatizo

Matukio mengine yaliyoambatana na adhimisho hilo ni pamoja na kuwasha Mshumaa wa Jubilei, kubariki Msalaba utakaotembezwa kwenye parokia zote kipindi chote cha maadhimisho kuelekea kilele, na tukio la kurusha hewani maarufu 'Njiwa wa Amani'-kama ishara ya kusambaza amani, upendo na Habari Njema kwa mataifa.

Tangu kuanzishwa kwake mpaka sasa, Jimbo Katoliki Singida limefanikiwa kuwa na Parokia 29, Waamini 186,797, Vigango zaidi ya 361, Makatekista 583, Mapadre wanajimbo waliopadrishwa 76 ambao kati yao ni Askofu wa sasa wa Jimbo hilo, Mhashamu Edward Mapunda.

Mapadre wengine waliopo ni kutoka Mashirika 32 yanayofanya kazi ndani ya Jimbo hilo, pia Maaskofu 3 (Askofu Bernard Mabula 1972-1999; Desiderius Rwoma 1999-2015, na Edward Mapunda 2015 mpaka sasa.

Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa Mashirika ya watawa wa Kiume na Like kufikia 30, Hospitali 4, Vituo vya afya 3, Zahanati 9, Seminari ndogo 3, Sekondari 7 na Shule za Msingi 12.

Imeelezwa, pamoja na mambo mengine, Jimbo hilo pia mpaka sasa lina Vyuo 6, Kituo cha Kichungaji 1, Vituo vya walemavu na wazee 3, watoto yatima 1 sambamba huduma nyingine za kiroho na kijamii.
Share To:

Post A Comment: