Na Mwandishi wetu,Geita


NAIBU  Waziri wa Maji,Mhandisi MaryPrisca Mahundi (MB) amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita Mhandisi Frank Changawa kuhakikisha mkandarasi wa awali aliyekuwa anatekeleza mradi wa Nyamtukuza Petty and Company (Ltd), kurejesha pampu ya mradi huo aliyorudishiwa kwa ajili ya matengenezo madogo ili iweze kufungwa na wananchi waendee kupata huduma ya majisafi na salama.  


Mhandisi Mahundi ametoa kauli hiyo alipokuwa anakagua utekelezaji wa mradi huo ambao umechukua muda mrefu kukamilika kutokana na wakandarasi kushindwa kukamilisha mradi kwa wakati hadi mkataba ulipovunjwa na kazi ya utekelezaji kuchukuliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA).


“Ninawapa siku saba (GEUWASA) kuhakikisha pampu iliyochukuliwa na Mkandarasi kwa ajili ya matengenezo inarejeshwa haraka ili ije ifungwe kwenye mradi kama mchoro wa awali unavyoonesha kufunga pampu mbili ili moja ikipata hitilafu, basi nyingine iendelee kufanya kazi, wananchi waendelee kupata huduma ya maji”, amesema Mhandisi Mahundi


Aidha alisusitiza  kuwa ndani ya siku hizo saba kupatiwa ripoti ya pampu hiyo kama imerejeshwa.


Amesema wananchi wengi nchini hususani wa maeneo ya vijijini  wanahitaji maji na hivyo kuwataka watekelezaji wa miradi hiyo kukamilisha kwa wakati unaotakiwa ili wananchi wapate huduma wanayostahiki.   


Aidha, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA) na watendaji wake kwa kuweza kutekeleza mradi huu ambao hapo awali ulikuwa kati ya miradi kichefuchefu kwa kutokamilika kwa wakati na sasa mradi umefikia hatua za mwisho na baadhi ya wananchi wa Nyamtukuza wameanza kupata huduma ya majisafi. salama na yenye kutosheleza. 


Mradi wa Nyamtukuza kwa sasa unatekelezwa na GEUWASA kwa kutumia wataalam wa ndani (Force Account) na umegharimu shilingi bilioni 11 ambapo kwa kutumia watalaam hao wa ndani serikali imeweza kuokoa shilingi bilioni 4 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi machi, 2021.


Mwisho.

Share To:

Post A Comment: