Wednesday, 24 February 2021

ALIYEPIGWA NA MTENDAJI HAYDOM AHUKUMIWA MIEZI MITATU JELAMKAZI wa Kijiji cha Ngwandakw Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, Rose Danielson aliyepigwa na ofisa mtendaji wa Kijiji cha Haydom, Adela Kente amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela au kulipa faini ya sh200,000 na fidia ya sh100,000.

Hata hivyo, mtendaji huyo wa kijiji hicho cha Haydom Adela baada ya kumpiga Danielson alisimamishwa kazi na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga kwa kudaiwa kupigana hadharani kinyume na utumishi wa umma.

Rose amesema hukumu hiyo imetolewa juzi alasiri kwenye mahakama ya mwanzo Dongobesh, baada ya kukutwa kwenye eneo la kazi na kisha kupigwa kwenye sikukuu ya mapinduzi ya Zanzibar Januari 12 mwaka huu. 

"Nililala ndani nikanyimwa karatasi ya matibabu na kunyimwa dhamana kisha nikafunguliwa mashtaka mahakamani ili hali mimi ndiye ambaye nilipigwa na huyo mtendaji wa kijiji," amesema Rose.

Hata hivyo, Rose amesema atashirikiana na taasisi za haki za binadamu ili akate rufaa kwenye mahakama ya wilaya hiyo kwani alipigwa na mtendaji huyo kisha yeye akashtakiwa mahakamani.

Amesema baada ya yeye kupigwa na kujeruhiwa na Adela alitegemea angeshtakiwa lakini haikuwa hivyo ila yeye ndiye ameshitakiwa mahakamani na kuhukumiwa.

"Ninamshukuru mbunge wa jimbo Flatei Maasay kwani nilipopigwa nilikosa msaada na pia namshukuru Mkurugenzi wa halmashauri Kamoga kwa kumsimamisha kazi Adela baada ya kunipiga," amesema Rose.

Amesema yeye hakuwa mkazi wa kijiji cha Haydom anaishi kijiji cha Ngwandakw' amepigwa kutokana na kudaiwa mchango wa madawati na kisha kushtakiwa hivyo anauliza haki ipo wapi.

Amesema baada ya kupigwa na mtendaji huyo japokuwa alimweleza kuwa yeye hapaswi kulipa mchango huo kwani siyo mkazi, alilazwa siku mbili kituo cha polisi na alinyimwa dhamana na hakupewa fomu namba tatu ya matibabu (PF3).

Amesema baada ya kupambaniwa na ndugu zake na kupata matibabu hospital ya Haydom alipelekwa mahakamani na kisha kushtakiwa kwa kumpiga Adela.

"Tulipeleka washahidi wanne mahakamani wakatoa ushahidi wao kwenye chumba kimoja ila haukuzingatiwa na siku hiyo hiyo baada ya ushahidi kutolewa baada ya saa moja hukumu ikatolewa sehemu ya wazi, " amesema Rose.

Amesema Adela alikuwa anatamba kuwa "Hawa wamburu hawataniweza subirini hukumu nitashinda na kazini nitarudi niwanyooshe vizuri." 

Akisoma hukumu ya kesi hiyo ya jinai namba 10 ya mwaka 2020, hakimu wa mahakama ya mwanzo Dongobesh, Julliet Mbise amesema Rose ametenda kosa la shambulio la kuzuru mwili Januari 12 mwaka 2021.

Rose alilipa faini ya sh200,000 na fidia ya sh100,000 kwa Adela hivyo kuepuka kwenda magereza kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela.

Mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu ilizunguka 'clip' kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha Adela akimpiga Rose kwa kile alichosema kutotoa mchango wa kununua madawati ya shule.

 

No comments:

Post a Comment