Saturday, 9 January 2021

RIDHIWANI KIKWETE AWAHAKIKISHIA WAFANYABIASHARA KUMILIKI VIZIMBA SOKO LA KISASA BWILINGUNA ANDREW CHALE, CHALINZE


MBUNGE Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete amewahakikishia Wafanyabiashara waliopisha ujenzi wa soko jipya la Bwilingu-Chalinze kuwa watapewa kipaumbele bila wasi punde ujenzi wa soko hilo utakapo kamilika.


Mbunge amesema hayo wakati wa ziara maalum ya Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango  inayotembelea miradi mbalimbali ya Halmashauri ya Chalinze mapema leo. 


Ridhiwani Kikwete amewahakikishia Wafanyabiashara hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa soko hilo, Shabani Mazengo kuwa ni shabaha yake kuona wanyonge waliojitolea kupisha ujenzi huo wanaenziwa kwa kupewa  nafasi ya kipekee kwenye soko hilo. 


Akiongea na wafanyabiashara hao akiwa na viongozi wenzake Mhe. Ridhiwani Kikwete alisema: 


"Wafanyabiashara waliokuwa hapa awali kuamua wenyewe kuvunja vibanda vyao kwa hiyari ambao wanapata 180, ndio wawe wa mwanzo kupewa nafasi hapa kisha wengine ndio wafuatie" Alisema Ridhiwani Kikwete.


Mbunge aliongeza kuwa: "Kwa sasa soko lipo katika hatua nzuri hadi mwezi wa Nne mwaka huu linatarajiwa kukamilika na litakuwa la kisasa zaidi" alisema Ridhiwani Kikwete.


Ridhiwani Kikwete alieleza kuwa ujio wa soko hilo ni baada ya Rais  Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kutoa maagizo kuwa miji yote mikubwa iwe na  masoko, Hospitali kwa maana (Vituo vya afya), hivyo wao kama halmashauri ya Chalinze wanaendelea na utekelezaji wa ilani kwa soko hilo.


"Maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ambapo pamoja na yote yana nia njema ya kuongeza mapato ndani ya Halmashauri yetu ya Chalinze na ustawi wa Wananchi wetu ambao watapata fursa ya huduma bora ndani ya soko  hili" Alisema Ridhiwani Kikwete.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Geoffrey Kamugisha alisema  wametembelea kujionea miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa soko hilo la kisasa na choo.


"Kamati tumetembelea na ujenzi huu ambao kwa Soko unagharimu kiasi cha Tsh. Milioni 449. Tunapongeza hatua kubwa iliyofikiwa hivyo tunaomba mkandarasi kuhakikisha ubora wa kazi na mapendekezo yaliyotolewa katika ujenzi yanazingatiwa." Alisema Kamugisha.


Ziara hiyo pia iliendelea kwa kamati hiyo ya Uchumi, Fedha na Mipango pia ilitembelea uzio wa Kituo cha Afya Chalinze na kumalizia ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Chalinze la Wakulima na Wafugaji katika viwanja vya Nane Nane, Morogoro.


End.

No comments:

Post a comment