Wednesday, 30 December 2020

Waziri Jafo: Natamani kuona Halmashauri zinajitegemea

 


Na. Angela Msimbira TAMISEMI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe, Selemani Jafo amesema ndani ya miaka mitatu ijayo matamanio yake ni kuona Halmashauri zinajitegemea zenyewe kupitia mapato ya ndani na kwamba ifike muda ziwe zinalipa watumishi wake mishahara. 


Waziri Jafo ameonyesha matamanio hayo leo wakati alipotembelea ujenzi wa mradi wa Government City Complex  katika eneo la Mji wa Serikali Mtumba unaogharimu  kiasi cha shilingi Bilioni 59.3 hadi kukamilika kwake ambapo ametumia nafasi hiyo kulipongeza jiji la Dodoma kwa kutekeleza kwa kutumia mapato yake ya ndani na si fedha za serikali.


Amesema hakuna halmshauri yoyote iliyofanya uwekezaji mkubwa nchini kama uliofanyika katika Jiji la Dodoma huku akieleza kuwa sasa analiona jiji hilo kupitia viongozi wake kuwa wapo kwenye sura hiyo anayoitamani.


 “Hakuna halmashauri yoyote iliyofanya uwekezaji mkubwa  kama huu hivyo nawapongeza jiji la Dodoma, nataka  jengo hili liwe kielelezo na kama nilivyosema mimi matamanio yangu nataka nione halmashauri zinazoweza kujitegeme zenyewe ifike muda halmashauri iseme hata nikiwa na watumishi wangu nitawalipa mimi mwenyewe natamani itokee ndani ya miaka mitatu ijayo,” amesema  Waziri Jafo.


Ameendelea kufafanua kuwa  analiona Jiji la Dodoma lipo kwenye sura hiyo kupitia hoteli hiyo kubwa ya mikutano iliyojengwa katika Mji wa Serikali.


“Nikiangalia hoteli kubwa ilivyo kuwa mjini ya ghorofa 11 nikiangalia soko lenu la Dodoma nikiangalia eneo la maegesho ya magari Nala, eneo la mapumziko na michezo Chinangali, Stendi ya Dodoma, ninapata uhakika kwamba halmashauri ya jiji la Dodoma inaenda kujitegemea,”amesisitiza Waziri Jafo.


 Ameuagiza uongozi wa jiji la Dodoma kuhakikisha wanakwenda kusimamia kazi hiyo kwa kiwango cha juu ili iwe nzuri ambapo  mtu akija ajifunze  na kumtaka mkandarasi  kutulia na kufanyakazi kwa uangalifu mkubwa. 


Amesema anahitaji jengo hilo kuwa kielelezo na kama nilivyosema mimi matamanio yangu ni kuona halmashauri zinazoweza kujitegemea zenyewe na ifike wakati ziwe zinalipa wafanyakazi wake kupitia fedha za ndani”


Amemuagiza mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ikiwa ni pamoja na mshauri wa mradi huo anayehusika na kazi ya michoro kuhakikisha ifikapo siku ya jumatatu awe amekamilisha kazi na asiwe kikwazo cha kuchelewesha mradi.


Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Jiji Joseph Mafuru amesema mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi  Bilioni 59.3 ambapo kwa awamu mbili ambapo ya kwanza ni ujenzi wa jengo la Tower B lenye ghorofa tano na kumbi za mikutano tano zenye uwezo wa kuchukua watu 1297.

No comments:

Post a Comment