NA NAMNYAK KIVUYO, DODOMA.


Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendheleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe amewapongeza viongozi na watumishi wa huduma za chanjo ngazi zote nchini kwa  utendaji bora wa utoaji wa chanjo kwa bidii na kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa kitaifa na kimataifa yanafikiwa.


Profesa Mabula alitoa pongezi hizo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa tathimini wa huduma za chanjo Tanzania unaofanyika kwenye ukumbi wa Mt. Gasper jijini Dodoma.


"Niwapongeze kwa jitihada zenu na kuifanya nchi kufanikiwa katika utoaji wa huduma za chanjo kwa kuvuka kiwango cha asilimia 90 kilichowekwa kimataifa, hivyo nawataka mkubaliane na kupanga mbinu na mikakati ya kudumisha na kuboresha zaidi viwango vya chanjo nchini,”Alisema Prof Mabula


Alieleza licha Mafanikio hayo Serikali kupitia Wizara yake itaendelea kudumisha  kiwango cha chanjo nchini na ana uhakika takwimu za mwaka 2020  zitakapotolewa na Shirika la Afya Duniani(WHO)  itafikia asilimia 98 au zaidi.


Aidha aliwaagiza viongozi wa afya ngazi za Mikoa na wilaya  kuhakikisha kuwa huduma za chanjo zinapewa kipaumbele  ili usitokee tena mkoa utakaoshindwa kudumisha kiwango kilichofikiwa kwani ili watoto waendelee kuwa na afya njema hakuna budi kuwapa chanjo bora za kuwakinga dhidi ya maradhi.


"Nchi yetu imekuwa na utekelezaji wa mkakati wa Fikia kila Wilaya,Fikia kila mtoto apate chanjo,nawasisitiza waratibu wa huduma za chanjo kuhakikisha kuwa mikoa inayofanya vibaya inatumia mkakati huu ili  kuhakikisha kuwa watoto na walengwa wote wanafikiwa katika kupata haki yao ya msingi ya chanjo," Alisema


Sambamba na hayo aliwashukuru wadau wote wa maendeleo kwa michango yao mbalimbali  katika kuhakikisha kwamba watoto  wanapatiwa chanjo bora  ambayo inaleta kinga dhidi ya maradhi ambayo yanaweza kusababisha ulemevu na vifo kwa watoto.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI  Dkt. Ntuli kapologwe aliwapongeza Waganga Wakuu wa Mikoa pamoja na waratibu wa huduma za chanjo nchini kwa kuwa kinara wa utoaji wa chanjo na kuweza kuwafikia walengwa wote nchini na kuongoze kuwa TAMISEMI inaipa uzito mkubwa suala la chanjo kwani kinga ya mtoto inaanza na chanjo.


Naye Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali ambaye pia ni  Mkurugenzi wa Idara ya kinga Kutoka Wizara ya afya, Dkt. leonard Subi alisisitiza kuwa wizara ya afya inasimamia ubora na usalama wa huduma wanazozitoa hasa upande wa chanjo ambao mara kadhaa umekua na mapokeo tofauti,hivyo amesisitiza kuwa wizara ipo makini zaidi na afya za wananchi


Hata hivyo Mwakilishi wa wadau wa maendeleo ambaye anatoka WHO Nassoro Mohamed  aliipongeza Wizara ya afya pamoja na viongozi wa mikoa kwa kuhakikisha watoto wote nchini wanafikiwa  licha ya changamoto za hapa na pale hivyo kama wadau wanashiriki ili kuhakikisha Serikali inafikia malengo waliyojiwekea katika kutoa huduma za chanjo.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: