Wednesday, 9 December 2020

Rais Magufuli Aagiza Mkurugenzi Aliyenunua Gari la Milioni 400 Asimamishwe Kazi

 


 Rais John Magufuli amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Geita, – Mhandisi Modest Apolinary kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za serikali.

Amemtaka Waziri Jafo kufanya hivyo haraka iwezekanavyo, ikiwa ni kazi yake ya kwanza mara baada ya kuapishwa hii leo.

Amesema hajafurahishwa na kitendo cha Mkurugenzi huyo wa halmashauri ya Mji Geita kununua gari lenye thamani ya Shilingi Milioni 400 wakati wanafunzi hawana madawati.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo Ikulu Chamwino jijini Dodoma mara baada ya kuwaapisha Mawaziri 21 pamoja na Naibu Mawaziri 23.

Amemuagiza Waziri Jafo kufuatilia changamoto mbalimbali ndani ya Wizara yake ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya fedha za serikali.

"Tamisemi kuna matumizi mabaya ya fedha Jafo (Suleiman- Waziri wa Tamisemi) umefanya vizuri sana lakini kwenye kudhibiti fedha bado, nimefikiria sana kukurudisha au kutokukurudisha. 

"Hapo nataka kusema ukweli tuelewane hili la matumizi mabaya. Unakuta mkurugenzi ananunua gari la milioni 400 fedha tumehangaika nazo kuzipata wananchi, watoto wanachangishwa unakuta madawa hayatoshi. Nataka  kazi yako ya kwanza kwenda kumsimamisha mkurugenzi wa Geita ndio kazi yako ya kwanza ukaanze nayo. "amesema Rais John Magufuli.

No comments:

Post a Comment