◊ Atoa onyo kwa kampuni zinazohujumu miundombinu ya TCCL

◊ Watakaoiba nyaya za shaba za TTCL kuhusishwa na uhujumu uchumi

 

Na Prisca Ulomi, WMTH

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amezipa siku 30 taasisi za umma zinazodaiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kulipa madeni kwa Shirika hilo ili liweze kujiendesha, kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma ya mawasiliano ya sauti na data kwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi ili kukuza uchumi na kuchangia pato la taifa

 

Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati wa ziara yake alipotembelea TTCL kwa lengo la kufahamiana na kuzungumza na wajumbe wa Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wa TTCL, Dar es Salaam ambapo aliambatana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo A. Mathew na Mejimenti ya Wizara hiyo

 

Ameongeza kuwa zaidi ya taasisi 20 za Serikali zinadaiwa na TTCL zaidi ya kiasi cha shilingi bilioni 30 ambapo zipo taasisi zinatumia huduma za mawasiliano za TTCL na zinakusanya mapato ya zaidi ya shilingi bilioni moja kwa mwezi ila hawako tayari kulipa huduma za TTCL

 

Vile vile, ametoa onyo kali kwa kampuni zinazohujumu miundombinu ya TTCL ili ishindwe kutoa huduma za mawasiliano kwa wateja wake kuwa waache tabia hiyo mara moja na wafanye biashara kwa misingi ya ushindani, vinginevyo Serikali itawachukulia hatua kali

 

Aidha, amesisitiza kuwa kwa watakaoiba nyaya za shaba za TTCL na kuuza kama chuma chakavu nao waache mara moja kwa kuwa watahusishwa na uhujumu uchumi kwa kudhoofisha utendaji kazi wa TTCL na kwa watakaobainika watachukuliwa hatua kali na Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama

 

Amewataka watendaji wa Wizara kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kufanya utafiti na tathmini ya kubaini mchango wa Sekta hii aidha wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja katika kukuza uchumi na kuchangia pato la taifa kwa kuwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wanachi wanatumia huduma za mawasiliano ya data na sauti na kuendesha shughuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii kwa kutumia TEHAMA

 

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo A. Mathew amewataka watumishi wa TTCL kuwa wabunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea na wajenge utaratibu wa kufuata na kuwahudumia wateja huko waliko badala ya kusubiri wateja kuwafuata ofisini

 

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amesema kuwa amepokea maelekezo ya Waziri, Dkt. Ndugulile na ametoa rai kwa watumishi wote wa TTCL kujituma ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya mawasiliano yenye kasi ya brodibandi kutoka asilimia 49 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2025

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Share To:

msumbanews

Post A Comment: