Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Kuimarisha Maadili na Usaidizi kwenye Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi (WoLaoTa), Samwel Olesaitabau Lukumay , akizungumza na waandishi wa habari jana (hawapo pichani) kuhusu Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwakumbuka wastaafu walau kwa nafasi 2 za uwakilishi kwenye Bunge lijalo.


Na Godwin Myovela, Singida


TAASISI ya Kuimarisha Maadili katika Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi Tanzania (WoLaOTa) imemsihi Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwakumbuka wastaafu walau kwa nafasi 2 za uwakilishi kwenye Bunge lijalo.

Akizungumza na vyombo vya habari  mkoani hapa jana, Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Samwel Olesaitabau  alisema kwa kufanya hivyo ni dhahiri atakuwa ameonyesha ishara ya kutambua mchango mkubwa uliotolewa, na unaoendelea kutolewa na wastaafu kama hazina katika ujenzi wa Taifa. 

"Kwanza itakuwa ni asante kwa wastaafu, lakini itapendeza zaidi sauti ya kundi hili muhimu ikawakilishwa pale bungeni kwa ustawi na maslahi mapana ya wastaafu wote," alisema Olesaitabau.

Akizungumzia hali ya uchaguzi mkuu uliopita, aliwapongeza watanzania kwa utulivu na ukomavu wa kisiasa walioonyesha katika kipindi chote cha mchakato wa zoezi hilo.

Aidha, kwa namna ya pekee alivipongeza vyombo vyote vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Polisi kwa namna walivyoonesha weledi wa hali ya juu kwenye kuimarisha amani na utulivu, wakati wakitekeleza majukumu yao.

Alisema kama Taasisi isiyo ya kiserikali inayoshughulikia maadili kwa watumishi, inatoa pongezi za dhati kwa ushindi wa kishindo na heshima alioupata Rais Magufuli na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kipindi kingine cha awamu ya pili.

Olesaitabau aliwakumbusha viongozi hao wakuu, akiwemo Rais wa Zanzibar Dkt. Ally Hussein Mwinyi kwamba ushindi walioupata ni deni ambalo malipo yake ni kuonyesha kwa vitendo utumishi uliotukuka kwa mustakabali chanya wa 'Maendeleo ya Tanzania'.

Aidha, kwa upande wa vyama vya upinzani, Taasisi hiyo imevitaka kutafakari kwa kina na hatimaye kuutambua ushindi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

"Sio vema na wala haina afya kuanza kutunishiana misuli na vyombo vya dola. Hata uwanjani Refarii akishatoa ushindi kwa timu A, basi ile timu B kama haikuridhika wanaenda kwenye vyombo vya kutoa haki ili wapewe haki hiyo".

Pia viongozi wetu wakuu kama wazazi na walezi ifike mahali wakubali kukaa meza moja na wapinzani ili kuchambua na kurekebisha changamoto zilizojitokeza ili kuleta ustawi na tija kwa mwendelezo wa amani iliyopo, lakini pia kutoa fursa kwa vyama vyote kujipanga vema kwa chaguzi zijazo." alishauri Olesaitabau


Share To:

Post A Comment: