Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema dhamira yake ni kuijenga nchi katika uchumi wa kujitegemea, kwa kutekeleza miradi ya mikubwa ya kimaendeleo kwa fedha za ndani pasipo kutegemea wafadhili.

Alitoa kauli hiyo jana mkoani Geita wilayani Chato, wakati akiwahutubia maelfu ya wananchi na wanachama wa CCM katika Uwanja wa Mazaina kumsikiliza akiomba kura, pamoja na kueleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano.

“Wapo watu wana mawazo ya kupata fedha kutoka kwa wafadhili, hivi hao wafadhili wao hawataki kuishi huko kwao? Yaani wafadhili wakuletee wewe. Ukichukua fedha za wafadhili lazima utarejesha mara mbili, ndiyo maana tukaamua kutekeleza miradi yetu kwa fedha zetu, tunataka kuijenga Tanzania yenye uchumi wa kujitegemea,” alisema Dk. Magufuli na kuongeza:

“Nimekaa Wizara ya Ujenzi, Ardhi, pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, najua ukitegemea cha ndugu hufa maskini, maana yake wanataka kutunyonya, tunataka kujitegemea wenyewe.”

Alisema katika kipindi cha miaka mitano mambo mengi yamefanyika nchini ikiwamo ujenzi wa barabara, madaraja makubwa likiwamo la Busisi-Kigongo, ujenzi wa reli ya kisasa, Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano nchi imekutana na changamoto nyingi za kiuchumi, kiusalama, lakini serikali ilishikamana na kufanikiwa kuleta mafanikio.

Alisema: “Wakati naingia madarakani nchi yetu ilikuwa ya uchumi wa kimaskini, leo inatambulika ni ya uchumi wa kati, baada ya kuingia madarakani tumejenga zahanati 1,200 nchi nzima, vituo vya afya 487, hospitali 98 za wilaya, hospitali za mikoa 10, hospitali za rufani tatu na zingine zinakuja, haya yote ni mafanikio, lakini bajeti ya dawa imeongezeka kutoka Sh. bilioni 31 hadi Sh. bilioni 270.”

Alisema kwa kipindi cha miaka mitano serikali iliamua kujikita katika fedha zinazopatikana kuwekeza katika kuboresha sekta ya afya, ujenzi wa miundombinu, sekta ya elimu na ujenzi wa miundombinu.

“Katika miundombinu nyie ni mashahidi, kwenye vivuko Ziwa Victoria watu walikuwa wanakufa kwa sababu walikuwa wanatumia mitumbwi, tulipoingia madaraka tukasema haiwezekani tukaamua kutenga Sh. bilioni 152 kukarabati meli zote na kununua meli kubwa yenye uwezo wa kubeba watu 1,200 na tani 400 za mizigo. Lengo ni kuwakomboa wananchi kwenye usafiri,” alisema.

Dk. Magufuli alisema ameamua kujitoa maisha yake ya kiuongozi kama sadaka kwa Watanzania, kwa kufanya mambo ya kimaendeleo kwa kuwajali maskini.
Share To:

Post A Comment: