Mgombea Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mrisho Gambo amesema serikali imeshaanza kutatua kero ya maji taka  katika kata ya Olmoti yanayotiririshwa na kiwanda nguo cha A-Z.

Aidha amesema endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa mbunge wao at ashirikiana na serikali kuondoa kero ya miundombinu mibovu ya barabara na vivuko kwenye maeneo ya makorongo katika kata hiyo.

Gambo amesema hayo jana ikiwa ni siku ya kwanza ya kampeni yake  katika kata hiyo ambapo alipata fursa ya kutembelea mitaa mbalimbali ya kata hiyo kwa ajili ya kujionea changamoto zinazowakabili kabla ya kuanza mkutano wake wa hadhara.

"Nimeona kero kubwa ya maji taka yenye harufu mbaya yanayitiririshwa na kiwanda cha nguo cha A-Z kwenye maeneo yenu. Lakini nataka niwahakikishie kuwa kero hii imeshaanza kufanyika kazi na serikali kupitia mradi mkubwa wa maji wa bilioni 520 unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha. (AUWSA) ".

Kuhusu miundombinu mibovu ya barabara na vivuko kwenye maeneo yenye makorongo katika kata hiyo Gambo aliwaomba wananchi hao kumchagua awe mbunge wao ili aweze kushirikiana na serikali kutatua kero hiyo.

Naye mgombea udiwani wa Kata hiyo  Raphael Lomwiko amewaahidi wananchi hao kwamba wakimchagua atasaidiana na Gambo pamoja na serikali kutatua kero ya umeme, maji pamoja na  miundombinu katika sekta ya elimu.


Awali wananchi wa kata hiyo walimweleza Gambo kuwa wanakabiliwa na adha kubwa ya maji taka yenye harufu mbaya yanayotiririshwa na kiwanda cha nguo cha A-Z kilichopo kwenye kata hiyo pamoja miundombinu mibovu ya barabara na vivuko kwenye sehemu zenye makorongo.


Katika mkutano huo pia Gambo alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya CCM Dkt, John Magufuli na diwani Lomwiko.


Mkutano  huo pia ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali  CCM ngazi ya wilaya na mkoa, wabunge wateule wa viti maalum Mkoa wa Arusha pamoja na wagombea walioshiriki mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM katika jimbo la Arusha Mjini.

Mgombea Ubunge Mrisho Gambo anaendelea na Kampeni zake na kesho tarehe 13/09/2020 atakuwa katika Kata ya Terrat Uwanja wa Shule ya Msingi Mkonoo kuanzia Saa Nane Mchana.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: