NA GRACE CHARLES , SIHA


BODI ya Nafaka na Mazao mchanganyiko, (CPB), imeanza mchakato wa kufufua zao la ngano ambapo wameingia makubaliano ya awali  na wakulima wa zao hilo wilayani  Siha ya kununua ngano yao yote watakayozalisha kwa mkataba.



Makubaliano hayo yanayolenga kuwawezesha wakulima hao kuzalisha ngano nyingi na bora yalifikiwa juzi baada ya Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, Dkt Anslem Moshi kukutana na wakulima hao juzi kwenye ofisi za kijiji cha Ngarenairobi akiwa ameambatana na wataalam kutoka ofisini kwake, halmashauri ya wilaya ya Siha na benki ya NMB.


Dkt Moshi alisema jukumu lao kubwa ni kuweka mizania kwenye biashara ya mazao kwa kile alichoeleza kuwa tija ikiwa ndogo faida nayo huwa ndogo hivyo ameamua kumleta mtaalam wa kilimo ili abadilishane uzoefu na wakulima hao jambo litakalowasaidia kuzalisha kwa tija hivyo kupata bei nzuri sokoni.


"Sisi tunawapa soko la uhakika kuwa ukilima ngano yako tunanunua yote. Sisi tuna kinu pale Arusha kina uwezo wa kuichakata tani 120 kwa siku na mahitaji ya mwaka ni tani 36,000.Tuna uwezo wa kutafuta masoko tuweze kuuza ile itakayokuwa imezidi," alisema Dkt Moshi na kuongeza.


"Tuko katika pointi ambayo uamuzi ni wetu tuamue kuwa kwenye uzalishaji wa tija ili tuweze kushindana na wakulima wengine kwa kusaini mkataba wa kuzalisha ngano bora na nyingi,".


"Tusitegemee kutumia mbegu zilizotokana na mavuno yetu ya msimu uliopita itabidi tununue mbegu. Tuache kukimbilia mbegu za bei rahisi tunaenda kwenye kilimo cha kisasa hivyo matumizi yatakuwa makubwa na mapato makubwa,".

 

Moshi alisema kuwa kipengele cha ubora ndiyo wanakipa kipaumbele kwani ngano hiyo wanainunua kwa lengo la kuisindika na kutengeneza unga kwa ajili ya chakula kinachotumiwa na binadamu.


"Kwa upande wa mbegu tuna taasisi zetu za watafiti kama TARI wakishatafiti wanapeleka kwa mzalishaji tumeshaongea na ASA (Kituo cha Taifa cha kuzalisha mbegu) . Anasema atapeleka wapi mbegu sisi tumeshaongea na wakulima watazinunua,".


"Wakulima wanauliza watauza wapi ? Sisi tutanunua ngano yote sasa benki ya NMB tuko nao hapa na wao wanasema watawakopesha kwa kuwa sisi tumewahakikishia tutanunua," alisema Dkt Moshi.


Alisema kuwa wataalam wao watakuwa wanafanya kazi kwa karibu katikanhatua zote za  a kuhakikisha wanapanda mbegu waliyoshauriwa kuitumia na kufuata hatua zote muhimu mpaka inapokuwa tayari kwa ajiki ya kuuzwa.



"Kwa mliofika hapa nimeona mna ekari zaidi ya elfu 8.

Wale walio tayari twendeni pamoja wale wanaosubiri wakiona mmefanikiwa na wenyewe watajiunga. CPB tunataka uhakika wa malighafi wewe (mkulima) unataka uhakika wa masoko ndugu zangu twendeni, wakati ni huu," alisema Dkt Mosha huku wakulima wakimpigia makofi.


Wameunda kikosi kazi kinachojumuisha wataalam wa sheria, kilimo na biashara kutoka CPB, wawakilishi watatu wa wakulima na mwakilishi wa benki ya NMB ili waweze kupata bei ya kununua ngano hiyo baada ya kufanya tathimini ya gharama za uzalishaji.

Tume hiyo inaundwa na wataalam wa CPB wakiongozwa na  mkurugenzi wa mipango, Ezekiel Maige,  Mwanasheria, Neema Sovela, Meneja wa kanda ya kaskazini, Hiza Kiluwasa, Meneja wa kinu cha kusaga nafaka cha Arusha, Iddi Mkolamasa, afisa kilimo Ayoub Mchema , wawakilishi watatu wa wakulima na afisa Kilimo wa halamshauri ya wilaya ya Siha, Anselim Lema.


Kikosi kazi hicho kinatakiwa kifanyie tathmini suala la gharama za uzalishaji ambapo wakulima watakaokuwa tayari watajaza fomu maalum za kuonyesha nia ya kutaka kufanya biashara ambapo baada ya hapo watasaini mikataba.


"Tutakutana na (ASA) taasisi ya kuzalisha mbegu nchini ili tuone namna wataweza kuzalisha hizo mbegu. Sisi tutamdhamini ASA ili ninyi NMB  mumkopeshe ili aweze kuzalisha mbegu za kutosha kutoa kwa wakulima," alisema Dkt Moshi.


Mwakilishi wa benki ya NMB kanda ya Kaskazini, Oscar Rwechungura alisema kuwa wako tayari kukaa mezani na CPB na wakulima hao kwa ajilI ya kujadili kiwango chao cha riba ya mkopo ambayo alisema ni asilimia 17 kwa mwaka.



"NMB tuko tayari kutoa mikopo. Tutakuja kukaa pamoja kuangalia wastani wa gharama za kuzalisha ekari moja ni kiasi gani. Tukishajua tunaangalia una ekari ngapi tunawapatia mkopo," alisema Rwechungura aliyeambatana na meneja wa benki hiyo tawi la Siha, Frank Kilas.



Aliwashauri wakulima hao kukamilisha taratibu zao za kusajili umoja wao kwa kile alichoeleza kuwa kuna changamoto kubwa sana kwa kampuni kama CPB kuchukua mkopo kwa ajili ya kuwasaidia pembejeo wakulima mmoja mmoja hivyo ni vema wakulima wakakopa benki wenyewe.


"Tunachoweza kujadili hapa ni riba yetu. Na CPB wameshalileta kwetu kwamba hii riba ya kwetu ya kawaida tunaomba muipunguze kidogo tumewasikia tuko tayari kwa majadiliano," alisema Rwechungura.


kiongea kwa niaba ya wakulima wenzake , Sandewa aliwashukuru CPB kwa kuwaletea mpango huo ambapo aliomba mchakato wa kupitia mikataba na kukubaliana masuala ya muhimu ikiwemo bei yafikiwe mapema ili waweze kusaini mikataba.


"Tulipokutana na Naibu waziri wa Kilimo, Hussein Bashe tulieleza kilio chetu kikubwa ni soko. Tunawashukuru kuja kutuletea fursa hii. Kilimo cha mkataba ni kilimo cha tija. Hii itatuwezesha kukopesheka na mabenki tufanye kilimo kwa faida," alisema Sandewa.


Awali Mkulima, Daniel Mosha alisema wanavuna wastani wa gunia  nane kwa ekari moja hivyo akaomba wakaweze kukaa pamoja na CPB kuona kama itawezekana wanunua ngano yao kwa bei ya shilingi 850 inayotolewa na makampuni  yanayonunua shayiri.



Kiongozi wa wakulima hao, Felix Mosha alisema kuwa wanaelewa kùwa hatua yao ya kuzalisha kiwango kidogo cha ngano kulinganisha na mahitaji ya soko la ndani ndiyo imesababisha serikali kitoweka ushuru kwa ngano inayoingizwa toka nje.


Alisema kuwa hatua hiyo imesababisha ngano inayoagizwa kutoka nje kuwa na bei ndogo kuliko inayozalishwa hapa nchini.





MWISHO
Share To:

msumbanews

Post A Comment: