Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema lengo la Seriķali la kuwekeza katika mafunzo ya ufundi stadi ni kuhakikisha nchi inakuwa na rasilimaliwatu yenye ujuzi na maarifa itakayoshiriki katika uchumi wa viwanda  kwa maendeleo endelevu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Wilayani Ileje mkoani Songwe Waziri Ndalichako amesema katika kuhakikisha nchi inakuwa na uchumi wa viwanda Serikali inaendelea kuwekeza fedha za kutosha katika ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya wilaya na mikoa, ambapo mpaka sasa tayari vyuo 11 vya wilaya vimekamilika.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2019/20 Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika halmashauri 25 ambavyo ujenzi wake unaendelea.

Profesa Ndalichako amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda inaweza kufikiwa ikiwa kutakuwa na wataalamu wa kufanya kazi katika viwanda hivyo.

Amesema katika kuhakikisha hilo linafikiwa serikali imeendelea pia kutenga fedha za uhakika kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya mikoa pamoja  na kununua vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia ili kuviwezesha kutoa wataalamu wenye weledi.

Profesa Ndalichako amesisitiza kuwa mafunzo ya ufundi stadi ni mkombozi, suluhisho na muarobani wa changamoto ya ajira kwa vijana ndio maana Serikali ya Awamu ya Tano inasisitiza kuongeza fursa za ufundi stadi ili vijana waweze kujiajiri na kuongeza tija katika shughuli wanazozifanya ama kuanzisha viwanda vidogo.

Aidha, Profesa Ndalichako amewataka wazazi na walezi nchini kuhakikisha wanawapeleka vijana waliopo mitaani katika  vyuo hivyo ili waweze kupata ujuzi na maarifa itakayowasaidia katika kujiendeleza wenyewe kiuchumi na kushiriki katika kutimizi azma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe Breg. Jen. Mstaafu Nicodemus Mwangela ameishukuru Serikali kwa kukamilisha chuo cha ufundi Ileje kwani ni chuo cha kwanza cha VETA katika mkoa huo ambacho kinakwenda kuwasaidia vijana wa wilaya hiyo.

Breg. Jen. Mstaaf Mwangela amesema mahitaji ya vyuo hivyo nchini ni makubwa sana katika kipindi hiki kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi ya vijana ikilinganishwa na watu wazima kwani vijana ni aslimia 70, hivyo ni muhimu kutizamwa kwa lengo la kuleta maendeleo nchini na pia kuongezeka kwa idadi ya shule za Msingi na Sekondori ambazo zinazalisha vijana wengi wasiokuwa na kazi.

Amesema ili kuisaidia makundi hayo njia pekee ni kuwapatia ujuzi na maarifa itakayowasaidia kujiajiri ama kuajiriwa na kuwawezesha kushiriki katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ufundi Stadi Dkt. Pancras Bujulu amesema Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Ileje kina  uwezo wa kuchukua wanafunzi 120 kwa wakati mmoja na kimekamilika baada ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutoa zaidi shilingi milioni 228 kukamilisha ujenzi huo.
Share To:

Post A Comment: