Na John Walter-Manyara
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoa wa Manyara imewaomba watanzania kusaidia kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana  kwa Mmiliki wa kampuni ya JACO SERVICES GROUP John Stepheni Kabelinde anaedaiwa kutumia nyaraka feki kupata zabuni.
Taarifa iliyotolewa na mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara Holle Makungu leo Julai 9.2020 imeeleza  kuwa, mtu huyo  anatuhumiwa kwa kujipatia kandarasi yenye nambari za usajili TRD/RM/MYR/2019-20 toka Tanroads mkoani Manyara iliyohusu kufyeka nyasi pembeni mwa bara bara inayotoka Babati hadi Gehandu wilayani Hanang.
Makungu amesema John Stepheni Kabelinde maarufu kwa jina la Babu Joha huonekana mara kwa mara maeneo ya Sinza makaburini jijini Dar es Salaam ambapo  inasadikika ndipo anapoishi na kuendesha shughuli zake.
Ameongeza  kuwa uchunguzi walioufanya unaonyesha kuwa Babu Joha aliwasilisha nyaraka za kupotosha zilizomwezesha kuwashinsda wazabuni wengine tisa walioomba kazi hiyo.
Amesema kuwa mtuhumiwa huyo kupitia kampuni yake ya JACO SERVICES GROUP,  amekuwa akikwepa kulipa kodi mbalimbali za serikali hivyo kuangukia kwenye makosa ya kuhujumu uchumi wa taifa.
Ametoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Manyara na watanzania wote kupitia vyombo vya habari, kwamba popote watakapomuona Babu Joha watoe taarifa katika ofisi za TAKUKURU zilizopo karibu  au kupitia namba ya dharura 113  au kwa kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Manyara 0738150124-25
Aidha amezionya kamati za tathmini katika Taasisi nunuzi kutimiza majukumu yao kwa kuhakiki kila kampuni wanayoifanyia tathmini kuona uhalali wa nyaraka zilizowasilishwa na kujiridhisha iwapo kampuni husika inalipa kodi za serikali kwani kushindwa kufanya hayo ni matumizi mabaya ya madaraka kinyume cha kifungu cha 31cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwanamba 11/2007 na kwamba hatua zitachukuliwa dhidi ya wahusika.

Share To:

Post A Comment: