KLABU ya Yanga imesema itamkata Shilingi Milioni 1.5 kwenye mshahara wake wa Juni, winga wake Mghana, Bernard Morrison kwa kosa la kufanya mahojiano na chombo cha habari kinyume na utaratibu. 

Taarifa ya Yanga SC leo iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu, Wakili Simon Patrick imesema kwamba hatua hiyo inafuatia Morrison kukiuka kanuni za klabu kwa kuitisha na kufanya mahojiano na chombo cha habari bila kufuata utaratibu.

“Kanuni zetu zinazuia wachezaji kuongea na vyombo vya habari hovyo hovyo na mchezaji huyo alishaelezwa taratibu zote za Klabu na ameamua kukiuka taratibu hizo akiwa na nia ovu, Klabu inampa adhabu ya kukatwa Tsh. 1,500,000/= kwenye mshahara wake kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Klabu,” amesema Wakili Simon Patrick.

Amesema kitendo kilichofanywa na Morrison ni cha kuihujumu Klabu na kuibua taharuki kwa makusudi binafsi jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa.

“Uongozi unawakumbusha wachezaji wote na Umma kwa ujumla kwamba hakuna mchezaji mkubwa zaidi ya Klabu na hatutavumilia kitendo chochote cha utovu wa nidhamu cha mchezaji yeyote,” amesema. 


Aidha, Yanga imesema mchezaji huyo ana mkataba halali na klabu wa hadi Julai 2022 – taarifa ambayo inafuatia mchezaji huyo kudai mkataba wake unaisha mwezi ujao.


Mgogoro huu unaibuka wakati leo Yanga SC inateremka Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kumenyana na Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu.
Share To:

Post A Comment: