Na. WAMJW-DSM

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea kiasi cha shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini kutoka kwa wadau wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Akiongea wakati wa makabidhiano hayo Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ameishukuru TPSF kwa uratibu wao kwa sekta binafsi kuchangia vifaa tiba hivyo ili vituo vya afya kuwa na vifaa muhimu vya kutolea huduma

“Wizara ya afya pamoja na TAMISEMI kwa kipindi cha miaka mitano tumeimarisha upatikanaji  wa dawa, vifaa na vifaa kinga,hivyo tunaishukuru sekta binafsi kwa kukubali kuchangia kwa umoja wenu katika jitihada za serikali ili vituo vya afya kuwa na vifaa tiba”.

Aidha, Prof. Makubi amesema kuwa Serikali inahakikisha vituo vya kutolea huduma za afya nchini vinakuwa na vifaa muhimu vya kutolea huduma na huduma bora zinazotolewa kwa wananchi pamoja na huduma zipatazo 13 za kipaumbele ikiwemo huduma za mama na mtoto kwa kupunguzavifo vya mama na mtoto.

"Sisi kama watumishi wenu tunathamini michango yenu,kwakweli mmefanya kazi kubwa".

Prof. makubi alisema kwa kipindi cha miaka mitano Serikali imeongeza vituo vya kutolea huduma za afya kutoka 7014 hadi 8783 ambapo kuna ongezeko  la vituo 1769 zikiwemo zahanati 1198 na vituo vya afya 487 na hivyo wataendelea kuimarisha upatikanaji wa vitaa tiba na dawa.

Vifaa vilivyokabidhiwa leo vitaenda kuimarisha afya za wananchi kuanzia ngazi ya Zahanati na hospitali ambapo pesa halisi ni zaidi ya shilingi  milioni 150 na kiasi cha shilingi milioni 1.9 ni  vifaa kinga na vifaa tiba  vikiwemo vifaa vya huduma za dharura (ICU)
-Mwisho-
Share To:

Post A Comment: