Monday, 8 June 2020

RC Wangabo asaidia nguvu za wananchi katika utekelezaji wa mwaka wa mtoto Rukwa.

Katika kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya kusoma bila ya kutembea umbali mrefu ili kufika shuleni, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametembelea shule za msingi shikizi katika vijiji vya Majengo na Lyazumbi, Wilayani Nkasi ili kuendelea kuhamasisha umaliziaji wa shule hizo ili zisajiliwe na kuweza kufundisha wanafunzi wa kuanzia darasa la nne na kuendelea.

Shule hizo ambazo hivi sasa ujenzi wake umefikia katika hatua tofauti katika ukamilishaji umempelekea Mkuu wa mkoa huo kutoa miezi mitatu ili shule hizo ziweze kukamilika na kusajiliwa ili ziwe shule rasmi na hatimae kupunguza idadi ya vijiji visivyokuwa na shule za msingi kutoka vijiji 59 na kuwa vijiji 57.

Aidha, katika kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati amewaagiza watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha wanazifikia kaya zote na kila mdau wa maendeleo katika vijiji pamajona na kata ili kuweza kuchangia ujenzi huo huku Mh. Wangabo akitoa mifuko ya saruji 100 kwa shule hizo ikiwa ni kuunga juhudi za wananchi katika kumkomboa mtoto na shida za kutembea umbali mrefu.

“Mwanzoni mwa mwaka huu tulizindua kampeni ya kuhakikisha kwamba, tunamlinda mtoto, tunathamini haki za mtoto, na ninyi hapa mmetekeleza kwa vitendo, huyu mtoto ana manyanyaso mengi sana, hapa mmesema anatembea km 12 mpaka 15, huu ni unyanyasaji wa mtoto unaofanywa na wazazi wenyewe, na wengine hawaoni kwamba huyu mtoto anateseka, na mateso haya anayatoa mzazi,haoni nasema tu nenda, anamuachia kama kuku anavyoachiwa asubuhi na jioni anafunguliwa aingie,” Alisema.

Wakitoa taarifa katika nyakati tofauti mtendaji wa Kata ya Majengo na Mtendaji Kijiji cha Lyazumbi walisema kuwa lengo la wananchi hao ni kuendeleza ujenzi wa shule hizo ni kuhakikisha Watoto hawatembei umbali mrefu kwenda shuleni na pia kupunguza msongamano katika shule za vijiji vya jirani.


Wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa shule ya msingi Majengo iliyopo, Kijiji cha Majengo, Mtendaji wa kata ya Majengo Nuru Mtoro alisema kuwa wanafunzi hutembea umbali wa Km 12 kwenda na kurudi na hivyo mkuu wa Wilaya alishauri  kuanzisha madarasa matatu kwa nguvu za wananchi na kumaliziwa na mradi wa EP4R mwaka 2018.

”Hii shule ilianza na wananfunzi 120 tu, mpaka sasa tuna jumla ya wanafunzi 457, ambao ni kuanzia darasa la awali mpaka darasa la nne, ambapo kutokana na ongezeko la wanafunzi, mkuu wa wilaya akashauri tuongeze madarasa kutokana na Watoto kubanana na  kukosa jengo la utawala na hatuna nyumba ya mwalimu katika hili eneo, hali inayopelekea walimu kufanya shughuli zao chini ya miti na kipindi cha masika kujibanza kwenye ukuta,” Alieleza.

Naye Mtendaji wa Kijiji cha Lyazumbi Elizabeth Felix alisema kuwa shule ya msingi shikizi ya Kijiji cha Lyazumbi ilianzishwa mwaka 2016 kwa nguvu za wananchi waliolenga kuwaepusha Watoto kutembea umbali wa Km 12 kwenda na kurudi katika Kijiji cha jirani cha Paramawe ilipo shule mama na makao makuu ya kata ya Paramawe, Wilayani Nkasi.

“Shule Shikizi ya Lyazumbi ina madarasa manne, matatu yamekamilika, moja limepauliwa bado kuwekewa sakafu na ujenzi wa umaliziaji wa magebo, shule Shikizi ya Lyazumbi inajumla ya wanafunzi 412, waviulana 118 na wasichana 260 ambao ni darasa la kwanza hadi darasa la tatu, na wanafunzi wa darasa la awali 44, ambao wasichana ni 22 na wavulana 22,” Alisema.

No comments:

Post a Comment