Pierre NkurunzizaBaraza la Mawaziri nchini Burundi limesema kwamba linaongoza nchi hadi rais mpya atakapoapishwa.
Uamuzi huo ulifikiwa kufuatia mkutano uliyofanywa siku ya Alhamisi chini ya uongozi wa Makamu wa Rais wa kwanza Gaston Sindimwo.
Kufikia sasa bado haijabainika ni lini kiongozi mpya ataapishwa, japo katiba iko wazi kuwa Spika wa bunge la kitaifa Pascal Nyabenda alitakiwa kuapishwa kushikilia wadhifa wa Rais kwa kipindi cha mpito hadi Rais Mteule atakapoapishwa rasmi kuchukua hatamu ya uongozi.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema Rais Mteule, JeneralI Évariste Ndayishimiye, pia ni mgonjwa.
Mke wake alipigwa picha akitia saini kitabu cha maombolezo japo Ndayishimiye hajaonekana hadharani.
Chama cha mawakili nchini Burundi kimetoa wito wa kuapishwa mara moja kwa rais mteule.
Tovuti ya kibinafsi pamoja na vyombo vingine vya habari vimesema kuwa mawaziri waliifahamisha mahakama hiyo kuhusu nafasi iliyo wazi katika ofisi ya rais.
Mahakama ya Katiba sasa inasubiriwa kutoa uamuzi ni nani anastahili kuapishwa kuwa rais, ilisema taarifa iliyochapishwa na tovuti ya Iwacu.
Kwa mujibu wa katiba Spika wa Bunge, Pascal Nyabenda, anatakiwa kuapishwa kama kiongozi wa mpito.
Hata hivyo, Evariste Ndayishimiye wa chama tawala cha CNDD-FDD aliyechaguliwa Mei 20 anatakiwa kuapishwa mwezi Agosti.
Rais wa zamani, Sylvestre Ntibantunganya, ametoa wito Ndayishimiye aapishwe mara moja kama rais wa Burundi.
Huku hayo yakijiri kundi la upinzani linataka uchaguzi ufanywe upya.
Nkurunziza ni nani?
Pierre Nkurunziza amekuwa mwanasiasa wa Burundi na kuwa madarakani tangu mwaka 2005.
Bwana Nkurunziza, kijana wa aliyekuwa mbunge, alinusurika mauaji 1993 ya wanafunzi wa Kihutu katika chuo kiuu cha Burundi ambapo alikuwa mhadhiri na kujiunga na waasi wa FDD kundi ambalo baadae lilibadilika na kuwa chama tawala cha CNDD-FDD ambacho alikuja akawa kiongozi.
Alikuwa mwenyekiti wa chama tawala cha CNDD-FDD, hadi alipochaguliwa kama rais wa Burundi.
Baada ya makubaliano ya Amani ya Arusha kati ya serikali na waasi, Nkurunziza alitajwa kuwa waziri wa mambo ya ndani kabla ya bunge kumchagua kama rais Agosti 2005.
2015, Nkurunziza alichaguliwa katika uchaguzi uliokuwa na utata na chama chake kwa muhula wa tatu madarakani.
Wafuasi wake na wanaompinga Nkurunziza walikosa kukubaliana katika suala la ikiwa ilikuwa halali kwake kugombea tena na maandamano yakafuata.
Share To:

Post A Comment: