Maofisa wanne wa Baraza la usimamizi wa Mazungira (NEMC) wakiwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu  jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Na Karama Kenyunko 
MAOFISA wanne wa Baraza la usimamizi wa Mazungira (NEMC) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka tisa yakiwemo ya kughushi, kula njama, utakatishaji fedha na kuisababishia Mamlaka hasara ya Sh. Milioni 18.5..

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali Janeth Magoha akisaidiana na Stanley Lugola na Sofia Nyanda mbele ya Hakimu mkazi Mkuu Huruma Shaidi imewataja washtakiwa hao kuwa ni,  Deusdedith Katwale, Magori Matiku, Obadia Machupa ma Lydia Nyinondi ambae ni Mhasibu msaidizi wa Nemc

Katika shtaka la kwanza washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Juni Mosi 2016 na Julai 30, 2017 ndani ya jiji la Dar es Salaam na Dodoma, walikula njama ya kutenda makosa ya kughushi, kutoa nyaraka iliyogushiwa, kuisababishia mamlaka hasara na kutakatisha fedha.

Katika mashtaka ya kughushi imedaiwa kati ya Agosti Mosi 2016 na Septemba 6, 2017 huko Kinondoni ndani ya jiji Dar es Salaam na Mkoani Dodoma Mshtakiwa Katwale  alighushi ripoti ya kutathmini mazingira ya mradi wa  Kituo cha Mafuta cha Ibra General Enterprises lililopo kitabu namba 132 Block T Chadulu Area A Dodoma Kwa dhumuni la kuonesha kwamba tathmini ya mazingira juu ya mradi huo ilikuwa imefanyika huku akijua kuwa siyo kweli.

Pia mshtakiwa huyo anadaiwa kughushi kikao cha tathmini ambayo ni nyaraka ya 'Minutes for Technical Advisory Committee (TAC' kuonesha kwamba kikao hicho kilichofanyika huki mshtakiwa Lydia akidaiwa kuwa Julai 5, 2016 maeneo ya Ofisi za NEMC Kinondoni, alighushi risiti yenye thamani ya Sh milioni 18.5 kuonesha kuwa zimelipwa kwa NEMC.

Katika shtaka la tano, imedaiwa kuwa, kati ya Juni Mosi, 2016 na Julai 30,2017 katika Ofisi za NEMC Kinondoni, mshtakiwa Katwale aliwasilisha nyaraka ya uongo kwa Mkurugenzi wa NEMC kuhusu mradi wa mafuta wa Ibra General Enterprises kuonesha kuwa ukaguzi wa mradi huo  ulifanyika huku akijua kuwa siyo kweli.

Aidha, mwendesha Mashtaka Luoga, alidai Julai 5,2016, Matiku aliwasilisha nyaraka ya uongo ya risiti kwa Yunis Mfala.

Imeendelea kudaiwa kuwa, washitakiwa hao pia wakiwa watumishi wa NEMC walikiuka kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi Mazingira iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 na hivyo, kujipatia Sh milioni 18.5 kwa ajili yao.

Katika mashitaka ya kusababisha hasara, imedaiwa kati ya Juni Mosi, 2016 na Julai 30 2017 huko Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja wakiwa watumishi  wa Nemc wakiwa na nia ovu walisababisha Mamlaka hiyo hasara ya Sh milioni 18.5.

Katika shtaka la tisa la utakatishaji imedaiwa, Sikh nanmahali hapo washtakiwa hao walijipatia kiasi hicho cha fedha toka kwa Mfala ambaye ni mmiliki wa mradi wa kituo cha mafuta cha Ibra General Enterprises huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kughushi.

Washitakiwa wamekana mashtaka nankwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi katika kesi hiyo umekamilika na kwamba Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) ametoa kibali cha kusikiliza kesi hiyo.

Wakili wa utetezi, Rugemeleza Nshala alidai wanaomba dhamana kwa wateja wao kwa sababu Mahakama Kuu imeshatoa uamuzi kwamba mashitaka ya utakatishaji fedha yanadhaminika.

Hata hivyo upande wa mashtaka waliongoza na wakili Luoga ulipinga vikali hoja hiyo na kusema kuwa mashtaka ya utakatishaji fedha hayafahamiki na kwamba wanafahamu uwepo wa kesi ya kikatiba ambayo iliamuriwa na Mahakama Kuu na kuongeza kuwa, mahakama iliwapa muda wa miezi 18 serikali kufanya mabadiliko ya sheria iliyozuia dhamana kwa Washtakiwa wa makosa ya utakatishaji fedha kwamba yadhaminike na kabla ya hapo sheria iendelee kutumika kama kawaida.

Hata hivyo, Nshala alidai mahakama inayo mamlaka ya kutoa amri yoyote kuhusu dhamana ambayo ni haki ya kikatiba ya washitakiwa. 

Akitoa uamuzi, Hakimu Shaidi alisema licha ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi wa mashitaka hayo kudhaminiwa lakini pia imetoa masharti kwamba  jamhuri irekebishe sheria hiyo kwa miezi 18 hivyo maombi hayo ya dhamana kwa sasa si sahihi na kama mtu ataona si uamuzi sahihi aende Mahakama Kuu kwa ajili ya kufanya mapitio.

Amesema, mahakama ya kisutu imefungwa mikono haiwezi kutoa dhamana hivyo, washitakiwa wataendelea kubaki rumande  hadi Juni 18, mwaka huu kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.
Share To:

Post A Comment: