Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana imetaja kesi inayomkabili aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, dhidi ya maneno ya uchochezi yenye lengo la kujenga chuki kwa wananchi kwa Rais .
Kesi hiyo iliyosajiliwa 279/2016, imetajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi, Godfrey Isaya.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo imepangwa kwa ajili ya kutajwa na upande wa Jamhuri umeomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hata hivyo, alidai kuwa mshtakiwa alijidhamini mwenyewe katika kesi hiyo.
Lissu alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza katika kesi hiyo Agosti 6, 2016 na alisomewa mashtaka matatu ya uchochezi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Cyprian Mkeha (kwa sasa Jaji wa Mahakama Kuu).
Kesi hiyo ni ya tatu kati ya kesi nne za uchochezi zinazomkabili katika mahakama hiyo.
Awali, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi akisaidiwa na Paul Kadushi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa, ulimsomea mashtaka yake mbele Hakimu Mkeha.
Kadushi alidai kuwa Agosti 2, 2016, katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ilala, Dar es Salaam akiwa na nia ya kujenga chuki kwa wananchi dhidi ya Rais na serikali, alitoa maneno ya uchochezi
.
Hakimu Isaya amepanga kesi hiyo kutajwa tena Julai mosi, mwaka huu.



Share To:

Post A Comment: