Na Joachim Nyambo,Mbarali.
KALULUNGA BLOG: KAPUNGA RICE PROJECT LIMITED WAPO CHINI YA KAMPUNI ...Halmashauri ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imeitunuku tuzo ya Cheti Kampuni ya Kapunga Rice Project Limited kama ishara ya kutambua mchango wake katika kusaidia jamii baada ya kampuni hiyo kujenga kituo cha afya katika kijiji cha Kapunga Kata ya Itamboleo wilayani hapa.
Jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha afya liliwekwa na Makamu wa rais Samia Suluhu Hassan mwaka juzi na hatimaye uzinduzi wa kituo hicho ukafanywa na Mwenge wa uhuru katika mbio zake wilayani hapa mwaka jana na sasa kinaendelea kutoa huduma.
Akikabidhi cheti hicho kwa uongozi wa kampuni hiyo,Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali,Brown Mwakibete aliitaja Kampuni ya Kapunga Rice kuwa miongoni mwa wadau ambao kwa sasa wana mcahango mkubwa kwenye jitihada za Halmashauri za kuwaletea wananchi maendeleo.
Makamu Mwenyekiti huyo,alikabidhi cheti hicho Mbele ya Madiwani wenzake kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Mwaka lililofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya kutwa ya Rujewa iliyopo wilayani hapa.
Mwakibete alisema ni wakati kwa wadu wengine yakiwemo makampuni yanayofanya kazi wilayani hapa kutambua kuwa wanapaswa kuwa na ushirikiano ili kuwajengea uwezo wananchi kuishi kwenye mazingira rafiki kwa kuwaondolea changamoto zinazowakabili.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halimashauri hiyo,Kivuma Msangi alisema Halimashauri iko tayari kushirikiana na mdau yeyote atakayeonesha nia ya kuwasaidia wana Mbarali kwa kuwatatulia changamoto zilizopo pasipo kujali anataka kufanya yeye kama yeye au kushirikiana na Serikali.
Akipokea cheti hicho,Afisa Mahusiano wa Kampuni ya Kapunga Rice,James Maliki alisema waliamua kujenga Kituo cha afya cha Kapunga kilichogharimu jumla ya Shilingi milioni 750 baada ya kuona wakazi wakazi wa kijiji cha Kapunga wanalazimika kutembea umbali mrefu wa zaidi ya Kilometa 25 kufuata huduma za afya kutokana na kata yao kukosa sehemu ya huduma ya matibabu.
Maliki aliipongeza Halmashauri na uongozi wake kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo na kuahidi kuendelea kushiriki katika miradi mbalimbali lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano chini ya rais John Magufuli ya kuwaondolea kero wananchi.
Hata hivyo afisa hiyo alisema kuanza kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo kunakofanya na kampuni yao kwa majirani kunatokana na mahusiano mazuri baina ya pande hiyo yanayoonekana sasa na kwamba kwa muda mrefu kampuni ilikuwa ikitamani kufanya mambo mengi lakini milango haikuwa wazi kama ilivyo hivi sasa.
Aliitaja faida nyingine amabyo vijiji jirani vimeanza kuipata kutokana na uwekezaji wa kampuni hiyo kuwa ni pamoja na Kujifunza kilimo cha kisasa cha zao la Mpunga ambapo Mashamba ya Kapunga rice yanatumika kama mashamba darasa kwa wakulima jambo linalosababisha kuongezeka kwa uzalishaji kwa wakulima wa zao hilo.
Kiasi cha Shilingi milioni 750 kilitumika kwa shughuli za ujenzi wa majengo sambamba na kununua vifaa tiba kwaajili ya kituo hicho cha afya.

Share To:

Post A Comment: