Benki ya Exim yatangaza likizo ya malipo ya mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 160 kwa wateja wake ili kuwanusuru na athari za janga la COVID - 19.

Benki ya Exim imetangaza msamaha wa likizo ya malipo ya mikopo kwa wateja wake wakubwa, wa kati na wadogo walipo katika sekta zilizo athirika zaidi kiuchumi kutokana na athari za mlipuko wa ugonjwa wa virus vya Corona (COVID 19). Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na benki hiyo katika kuwasaidia kifedha wateja wake waliopo sekta ambazo zimeathiriwa zaidi na athari za mlipuko wa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Bw Jaffari Matundu alisema msamaha huo wenye thamani ya zaidi ya sh Bilioni 160 umeanza mwezi Juni mwaka huu, ukihusisha likizo ya malipo ya mikopo kwa wateja na nyongeza ya muda wa urejeshaji wa mikopo ili kusaidia wateja wa benki hiyo katika sekta mbali mbali kutokana na athari za janga hilo kwenye biashara zao.

"Benki inaelewa mahitaji ya wateja wetu wakati huu na tunafanya yote yanayowezekana kuwasaidia ili waweze kuvuka salama katika kipindi hiki kigumu. Jitihada hizi haziishii tu kwenye misamaha hii tunayoitoa bali pia kupitia huduma za ushauri kuhusu mikakati ya biashara ili kuhakikisha kwamba biashara za wateja wetu zinadumu na zinafanyika kwa mafanikio zaidi,'' alisema.

Kwa mujibu wa Bw Matundu msamaha huo unazingatia vigezo mbalimbali kwa kila mteja kwa kuwa athari za COVID-19 hazikuwa sawa katika sekta zote. "Tunafarijika kwa kuwa tayari wateja waliopo kwenye sekta zilizoathiriwa zaidi wameshaanza kusaidiwa. Mazungumzo na wateja wengine bado yanaendelea ili kutambua hatua mbali mbali zinazofaa kulingana na aina ya biashara, " aliongeza.

"Siku zote Benki ya Exim, tunaamini katika kufanya kazi kwa bidii leo kwa ajili ya kesho bora kwa wateja wetu, biashara zao na jamii kwa jumla, ni kwa mtazamo huo tumepitisha hatua kama hii katika wakati huu mgumu.Tunaendelea kujitolea kushughulikia mambo haya na kupata suluhisho sambamba na mamlaka pamoja na Serikali katika kuhakikisha uchumi wetu unaendelea kuwa thabiti wakati wa nyakati hizi ngumu. " alihitimisha.
Share To:

Post A Comment: