Na WAMJW - DSM

Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa wito kwa Wafanya kazi katika maeneo ya saluni kuchukua tahadhari ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona katika maeneo yao.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

"Kwa wale ambao wanasafisha nywele, kucha, wanafanya masaji, wanaosuka nywele, mchukue tahadhari kwasababu mpo katika hatari kubwa sana ya kuambukizwa lakini vile vile kuambukiza watu wengine maambukizi ya virusi vya Corona" alisema

Aliendelea kusema kuwa, Serikali inaendelea kuwakumbusha wafanya kazi wote katika maeneo ya saluni kuhakikisha wanaepuka msongamano pindi wanapokuwa katika majukumu yao, huku akisisitiza ni muhimu kwa kinyozi kuvaa Barakoa pindi ananyoa.

"Tunawakumbusha tena, kwa upendo kabisa, Tunawakumbusha muepuke msongamano ndani, awepo mtu anaenyoa na anaenyolewa na yule ambae ananyoa ahakikishe muda wote amevaa Barakoa, tunawaambia hivi kwasababu tunawapenda" alisema.

Kwa upande wake, Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, amewataka madereva wote wa vyombo vya moto hususan bodaboda na bajaj kuhakikisha wanavitakasa vyombo vyao vya usafiri kwa sabuni mara kwa mara ili kuua maambukizi ya virusi vya Corona endapo vitakuwepo.

Nae, Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) amesisitiza kuwa ili kupambana na ugonjwa huu watu wasichoke kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka ili kuepuka kupata maambukizi ya virusi vya Corona.

Uhamasishaji huu unafanywa kupitia kampeni hii ya “Mikono safi, Tanzania salama” inaratibiwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR kwa kushirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery unaendelea katika Jiji la Dar es Salaam.

Mwisho
Share To:

msumbanews

Post A Comment: