Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema  kuwa mamlaka nchini Kenya zimekuwa zikitangaza kuwa madereva wa Tanzania wanaotaka kuingia nchini humo wana maambukizi ya virusi  vya corona, jambo ambalo si sahihi.

Gambo amesema hayo na kueleza kuwa mbinu hiyo ya mamlaka za Kenya inalenga kuua soko la utalii mkoani Arusha na Tanzania kwa ujumla.

Katika taarifa yake aliyoitoa leo Mei 20, 2020 kiongozi huyo amesema amebaini hilo baada ya madereva 19 wa Tanzania waliotangazwa na Kenya kuwa na maambukizi kupimwa upya na kubainika hawana maambukizi ya virusi hivyo .

"Katika kujiridhisha tulichukua upya sampuli za baadhi ya madereva waliotoka Tanzania na kupimwa mpakani Namanga upande wa Kenya na kutangazwa na nchi ya Kenya kuwa ni POSITIVE , sampuli zilipopelekwa  Maabara zilionesha kuwa madereva hao kutoka Tanzania ni NEGATIVE 

"Baada ya kujiridhisha kwa kuwapima madereva wa Tanzania waliotangazwa wana Corona nchini Kenya ilihali hawana, Mkoa wa Arusha umejiridhisha kuwa, hizi ni mbinu za nchi ya Kenya kuua soko la Utalii katika mkoa wa Arusha na Nchi ya Tanzania kwa ujumla"  Amesema Mhe. Mrisho Gambo, RC Arusha

Amesema mkoa huo kwa sasa unaendelea kuchukua tahadhari kudhibiti maambukizi ya Corona kupitia Mpaka wa Namanga unaoziunganisha Tanzania na Kenya.

Amebainisha kuwa Mei 14, 2020 sampuli za madereva 44 mpakani hapo zilichukuliwa na kupelekwa Dar es Salaam katika maabara ya taifa ambapo majibu yanaonesha kuwa madereva 14 (11 wa Kenya, 1 wa Uganda na 2 kutoka nchi ambayo hakuitaja) kutoka Kenya walikutwa na maambukizi, huku 30 wakiwa hawana.

Amesema Majibu ya sampuli 23 za Mei 16, 2020 yalithibitisha madereva 10 wote Wakenya wana Virusi vya Corona na wengine 13 walikutwa hawana. Sampuli za Mei 18 bado zinaendelea kufanyiwa vipimo na majibu yatatolewa yakishapatikana. 



Share To:

Post A Comment: