MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameongoza mamia ya wakazi wa Iringa na vitongoji vyake kuulaza mwili wa marehemu, Dk Augustine Mahiga kwenye nyumba yake ya milele katika kijiji cha Tosamaganga, nje kidogo ya manispaa ya Iringa.

Dk Mahiga ambaye hadi mauti inamkuta nyumbani kwake Dodoma juzi, alikuwa Waziri wa Sheria na Katiba wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amezikwa katika makaburi ya Tosamaganga kwa heshima zote za serikali katika tukio lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa na serikali akiwemo Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Akson na Mkurugenzi wa Idara ya Usalam wa Taifa Diwani Athumani.

Katika salamu zao zilizotanguliwa na wasifu wake uliosomwa na Katibu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Profesa Sifuni Mchome, Makamu wa Rais alisema, Dk Mahiga atakumbwa kwa uchapa kazi wake, unyenyekevu na uzalendo wake wakati wote alipokuwa akilitumikia Taifa ndani na nje ya nchi kupitia nyadhifa mbalimbali alizokuwa nazo.

“Kutokana na umahiri wake katika masuala ya kidiplomasia, Dk Mahiga alikuwa mwakilishi mzuri wa Taifa katika masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa,” alisema.

Suluhu alisema Taifa limempoteza mtu mwenye mchango mkubwa na uzalendo wa hali ya juu ambaye historia yake itakumbukwa na vizazi vyote.

Awali akitoa salamu za bunge kwa niaba ya Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Naibu Spika wa bunge hilo, Dk Tulia Akson alisema bunge lilimfahamu Dk Mahiga kama mtu mwenye weledi, ufahamu, akili nyingi, mnyenyekevu, msikivu na mwenye upendo.

“Kama bunge tueleze masikito yetu makubwa, tumempoteza mtu aliyekuwa msaada mkubwa sana kwa shughuli za bunge na kiserikali,” alisema huku akitoa taarifa kwamba mke wa marehemu ameshindwa kuhudhuria mazishi hayo kwasababu yupo Nairobi nchini Kenya akiuguza mmoja wa watoto wao.

Dk Akson alisema watanzania wanayo mengi ya kujifunza kutoka kwa Dk Mahiga na ni muhimu na wao wakajiandaa ili siku watakapotangulia mbele za haki, watanzania wengine wajifunze mazuri kutoka kwao.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa alisema marehemu alijiunga na idara hiyo mwaka 1976 na anakumbukwa sana kwa rekodi alizoacha za kutekeleza majukumu kwa kuzingatia uzalendo wa nchi yake.

“Kwa niaba ya maafisa wote wa idara ya usalama nchini, niwape pole wanafamilia kwa msiba huu. Msiba huu sio kwa familia pekee yake, ni majonzi kwetu sote, wakati wote tukumbuke haya ni mapenzi ya Mungu, tukumbuke sisi sote tutapitia kipindi kama hiki,” alisema.

Kwa upande wake mwakilishi wa Jaji Mkuu, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Panterine Kente alisema idara ya mahakama imesikitishwa kuondokewa na kiongozi wake mahiri.

“Idara yetu itamkumbuka Dk Mahiga katika kipindi chote alichokuwa waziri wake,” alisema huku akimsifu waziri huyo kwamba amefariki akiwa mastari wa mbele kupigania maboresho ya wizara yake kupitia bajeti ya wizara yake iliyopitishwa na bunge hivi karibuni.
Akitoa salamu za pole kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi alisema; “Kwa niaba ya wana Iringa nitumie fursa hii kutoa pole kwa familia. Wana Iringa wamepata pigo kubwa, wamepoteza mtu wao, mkalimu, mwenye upendo, kiongozi, mwalimu na mtu mwenye mapenzi na Iringa.”

Kwa jinsi alivyokuwa mnyenyekevu, asiye na mabega ya kujiweza na mtu wa kujishusha, Hapi alisema Dk Mahiga amewaachia funzo viongozi waliopo kwamba sifa hizo ni muhimu katika uongozi.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walioongea kwa sharti la kutotaja majina yao walisema wameguswa na msibwa huo kwani Dk Mahiga ni mtu waliyemtegema kurudi baada ya bunge la jamuhuri ya Muungano kuvunjwa na kugombea ubunge kupitia jimbo la Kalenga.

“Baada ya kurudi kutoka umoja wa mataifa, Dk Mahiga aliingia katika siasa za Tanzania kwa kutupa karata yake katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015 lakini bahati haikuwa yake,” alisema mmoja wa wananchi hao wa jimbo hilo la Kalenga kilipo kijiji hicho cha Tosamaganga.

Alisema baada ya kukosa nafasi hiyo, Dk Mahiga hakukata tamaa na akajaribu kugombea ubunge jimbo la Iringa Mjini kupitia chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM) na kushika nafasi ya nne iliyomnyima uteuzi wa kuwania nafasi hiyo.

“Hata hivyo tumshukuru Rais Dk John Magufuli aliuona uwezo wa Dk Mahiga na wakati akikaribia kuunda baraza lake la mawaziri, akamteua kuwa mbunge kupitia nafasi zake 10 na kisha Waziri wa Mambo ya Nje kabla ya kumhamishia Wizara ya Katiba na Sheria hadi mauti inamkuta,” alisema.

Alisema wananchi wa jimbo la Kalenga alikozaliwa waziri huyo walikuwa na shauku kubwa ya kuona baada ya bunge hili kuvunjwa, anarudi nyumbani kwake Kalenga na kugombea ubunge wa jimbo hilo.


Share To:

Francis Godwin Mzee wa matukiodaima

Post A Comment: