Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amekagua ofisi mpya za Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu zilizopo eneo la Tazara jijini  Dar es Salaam na kuitaka Bodi hiyo  kujiandaa kulipa wanafunzi wakati wowote vyuo vitakapofunguliwa.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo  leo (Jumatatu, Mei 18, 2020) baada ya kukagua ofisi hizo  na kufanya kikoa cha pamoja na  menejimenti ya Bodi hiyo.


”Katika kipindi hiki ambapo vyuo vya elimu ya juu vimefungwa, HESLB ihakikishe inatumia muda huu kufanyia kazi changamoto zote za wanafunzi ili vyuo vitakapofunguliwa malipo ya mikopo ya wanafunzi yafanyike kwa wakati,” amesema Waziri Ndalichako

Kiongozi huyo  ameipongeza HESLB kwa kutekeleza agizo la Serikali la Kuhakikisha Taasisi zote za umma zinahamia kwenye majengo ya Serikali ili kupunguza gharama.

“Ninaamini hapa mtafanya kazi kwa utulivu na kutaongeza ufanisi katika kazi,” amesema Waziri Ndalichako.

Prof. Ndalichako pia alitumia kikao hicho kuwakumbusha watumishi wa HESLB kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Akiongea katika kikao hicho,  Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema HESLB ipo tayari kuwahudumia wanafunzi muda wowote vyuo vitakapofunguliwa kwa kuwa fedha zinazohitajika, mifumo na taarifa za wanafunzi zipo.

Badru ameongeza kuwa taasisi yake inakamilisha mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2020/2021 kwa kushirikisha wadau wakiwemo wanafunzi kupitia shirikisho lao, TAHLISO.

Kuhusu urejeshaji wa mikopo iliyoiva, Badru amesema TZS 160 bilioni zimekusanywa katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, Julai 2019 hadi Aprili 2020.

HESLB ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai 2005 ili kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi watanzania wasio na uwezo na pia kukusanya mikopo iliyoiva iliyotolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.
Share To:

Post A Comment: